Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua amesema Serikali ya Awamu ya 5 imerithi Uchumi mbaya kutoka katika awamu iliyopita na kuwataka wananchi kuwa na subira maana ndani ya siku 90 hadi 100 uchumi utaimarika
Akizungumza jana Jumapili katika mahojianona NTV, Gachagua alisema, "Hali ni mbaya sana, hakuna pesa katika Hazina, na kidogo tunachokusanya kinakwenda kwenye mishahara na unapaswa kufanya nchi iendelee hivyo tunahitaji kufanya mengi ili kuongeza uzalishaji,"
Aidha, kuhusiana na kupanda kwa bei ya Mafuta amesema, “Tunatafuta suluhisho la kudumu na endelevu. Itakuwa udanganyifu kwa watu wa Kenya kuendelea kutoa ruzuku ya mafuta kwa muda mfupi tu, halafu tunakwama kiuchumi”
Ameongeza pia kuwa, Uongozi wa Kenya Kwanza kwa sasa utajikita kukipa kipaumbele kilimo kama mbadala wa kunyanyua uchumi wao na kushusha bei ya chakula kama mahindi ambayo bei yake haikamatiki kwa sasa.
“Tutatumia muda mwingi, jitihada na fedha katika kilimo. Hii ndiyo njia pekee ya kwenda. Niwaambie Wakenya kuwa ndani ya miezi miwili au mitatu ijayo tutaanza kuona matokeo yake.
“Tumeshatoa maelekezo kwa Mamlaka ya Mapato (KRA) kwamba tunahitaji kubadilisha sheria ya kodi. Tunahitaji kuongeza wigo wa ukusanyaji mapato, tutaongeza uzalishaji wa bidhaa za mazao,” alisema Gachagua.