Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan umetangaza habari ya kugunduliwa makaburi 13 ya halaiki katikati mwa jimbo la Darfur huko kaskazini magharibi mwa Sudan.
Vita vya kuwania madaraka baina ya majenerali wa kijeshi nchini Sudan vilianza tangu tarehe 15 Aprili mwaka huu kati ya jeshi na vikosi vya msaada wa haraka. Juhudi zote za upatanishi wa kikanda na kimataifa za kumaliza vita na kuzileta pande zinazozozana kwenye meza ya mazungumzo zimeshindikana.
Hadi sasa, kumeshatangazwa usitishaji vita mara kadhaa nchini Sudan kupitia upatanishi wa kimataifa, lakini hakuna makubaliano yoyote yaliyoheshimiwa.
Kwa mujibu wa televisheni ya Al Jazeera, ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan umesema kuwa umepokea ripoti za uhakika za kugunduliwa makaburi 13 ya halaiki katika mji wa Al-Janina, ambao ni makao makuu ya jimbo la Darfur. Vita baina ya majenerali wa kijeshi vinasababisha hasara kubwa Sudan
Ripoti hiyo imesema kuwa, makaburi ya halaiki ni ya raia ambao wengi wao ni wa kabila la Masalit ambao hivi karibuni walishambuliwa na vikosi vya msaada wa haraka.
Huku hayo yakiripotiwa, taarifa nyingine zinasema kuwa, takriban raia 40 waliuawa jana Jumatano huko Nyala, makao makuu ya Jimbo la Darfur Kusini la Magharibi mwa Sudan, katika mashambulizi ya anga yaliyofanywa kwenye soko moja maarufu na vitongoji vya raia.
Duru za hospitali zimesema kuwa, ndege za kivita za jeshi la Sudan zilianzisha mashambulizi makali yaliyolenga makazi ya raia, ikiwa ni pamoja na vitongoji vya Al-Sad Al-Ali, Al-Riyadh, na Texas" mapema jana Jumatano.
Hayo yamethibitishwa na mtu mmoja aliyeshuhudia shambulio hilo wakati alipohojiwa na shirika la habari la Xinhua kwa njia ya simu na kuongeza kuwa, shambulio la anga lililenga pia soko maarufu la Al-Malaja huko Nyala."