Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majambazi wenye silaha wateka nyara watu 30 katika chuo kikuu cha Nigeria

B87F4B65 F17F 46A8 97C8 48149F0AB3CD.jpeg Majambazi wenye silaha wateka nyara watu 30 katika chuo kikuu cha Nigeria

Sat, 23 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Majambazi wenye silaha wamewateka nyara zaidi ya watu 30, wakiwemo angalau wanafunzi 24 wa kike, katika uvamizi katika na karibu na chuo kikuu kaskazini magharibi mwa jimbo la Zamfara nchini Nigeria.

Kwa mujibu ya mashuhuda, mapema Ijumaa, makumi ya majambazi walivamia kijiji cha Sabon Gida kwenye ukingo wa Chuo Kikuu cha Shirikisho nje ya mji mkuu wa jimbo la Gusau na kuvunja milango ya bweni tatu za wanawake na kuwateka waliokuwamo.

Shambulio hilo lilikuwa la kwanza la utekaji nyara mkubwa katika chuo kikuu tangu Rais Bola Ahmed Tinubu aingie madarakani, na kuahidi kukabiliana na changamoto za usalama nchini humo.

Wanajeshi walitumwa kutoka Gusau, umbali wa kilomita 20 na kuwakabili washambuliaji katika ufyatulianaji wa risasi lakini kundi la watekaji nyara liliwatorosha mateka huku kundi jingine likiwakabili wanajeshi.

Yazid Abubakar, msemaji wa polisi wa jimbo la Zamfara, alithibitisha shambulio hilo lakini alikataa kutoa maelezo zaidi, akisema maafisa wa usalama wanajitahidi kuwakomboa mateka hao.

Afisa mmoja wa jeshi alisema operesheni ya kijeshi inaendelea huku wanajeshi wakikabiliana na washambuliaji katika msitu ulio karibu na mji wa karibu wa Tsafe.

Zamfara ni mojawapo ya majimbo kadhaa kaskazini magharibi na katikati mwa Nigeria yanayotishwa na majambazi wanaovamia vijiji, kuua na kuwateka nyara wakazi pamoja na kuchoma nyumba baada ya uporaji.

Magenge hayo yana kambi katika msitu mkubwa unaozunguka majimbo ya Zamfara, Katsina, Kaduna na Niger.

Mnamo Februari 2021, majambazi walivamia shule ya bweni ya msichana katika mji wa Jangebe katika jimbo la Zamfara, na kuwateka nyara zaidi ya wanafunzi 300.

Wasichana hao waliachiliwa siku chache baadaye kufuatia malipo ya fidia ambayo ililipwa na serikali.

Nigeria inakabiliwa na changamoto lukuki za kiusalama, ikiwa ni pamoja na hujuma ya miaka 14 ya magaidi wakufurishaji wa Boko Haram kaskazini mashariki ambao wameua takriban watu 40,000 na kuwalazimisha wengine zaidi ya milioni mbili kukimbia makazi yao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live