Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaji ‘wajifungia’ kuamua ushindi wa Ruto

Majaji Data Majaji ‘wajifungia’ kuamua ushindi wa Ruto

Sat, 3 Sep 2022 Chanzo: Mwananchi

Ni saa 36 za kihoro kwa Rais mteule wa Kenya, William Ruto na mpinzani wake mkuu Raila Odinga wakati Mahakama ya Juu ya Milimani itakapotoa hukumu ya matokeo ya kura za urais yaliyompa ushindi wa Ruto.

Kihoro hicho hakiishii kwa wanasiasa hao bali kinawahusu wafuasi, mashabiki wao na watu wa mataifa mbalimbali wanaotaka kujua hatima ya kisiasa ya Kenya iliyofanya Uchaguzi Mkuu, Agosti 9, 2022 na matokeo yake kutangazwa Agosti 15 na Mwenyekiti wa Tume ya Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya, Wafula Chebukati.  

Ni saa 36 za kuamua kama Ruto ataapishwa Septemba 13, 2022 kuwa Rais wa Kenya au kinara wa Azimio la Umoja, Raila Odinga atapata fursa nyingine ya kuwania urais kama matokeo yatabatilishwa au atakwenda kustaafu siasa.

Majaji wa Mahakama ya Juu nchini Kenya wamejifungia kuandaa hukumu ya kesi iliyofunguliwa na Odinga na baadhi ya watu wakipinga matokeo ya urais yaliyotangazwa na IEBC.

Jaji Mkuu Martha Koome na majaji Philomena Mbete Mwilu, Mohamed Ibrahim, Dkt Smokin Wanjala, Njoki Susanna Ndung’u, Isaac Lenaola na William Ouko wanatarajiwa kutoa uamuzi wao kuhusu kesi ya kupinga ushindi wa Dk Ruto keshokutwa Septemba 5, 2022.

Katika matokeo yaliyotangazwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Agosti 15 mwaka huu, Ruto alishinda kwa kuzoa kura 7, 176, 142 (asilimia 50.49 ya kura) huko Odinga alipata kura 6, 942, 930 (asilimia 48.85).

Advertisement Jana Ijumaa, mawakili wa pande zote walihitimisha uwasilishaji wa ripoti zao za mwisho katika jitihada za kushawishi majaji hao saba kukubaliana na misimamo yao katika kesi hiyo.

Wakili Julie Soweto alizua taharuki katika mahakama hiyo alipocheza kanda iliyoonyesha jinsi raia wa Venezuela, Jose Camargo aliyedai kuwa ndiye aliyevuruga matokeo ndani ya mtandao wa IEBC.

Soweto alidai kuwa jina la raia wa kigeni lilikuwa kwenye Fomu 34A.

“Huyu ndiye mtu aliyekuwa akivuruga matokeo ndani ya mitambo ya IEBC. Hii ilifanyika Agosti 9 na tuliambiwa kuwa wageni hawa hawakuwepo.

“Tuliambiwa na wakili wa IEBC, Eric Gumbo, wageni hawakuingilia uchaguzi huu. Tuliambiwa kuwa hawakuingilia sava. Lakini katika Fomu hii ya 34A jina la Jose Camargo linaonekana wazi,” Soweto aliiambia mahakama hiyo.

Camargo alikuwa mmoja wa raia watatu wa Venezuela waliokamatwa katika Uwanja wa Ndege wa JKIA wiki chache kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Watatu hao walikamatwa na maofisa wa usalama katika uwanja kwa kupatikana na vibandiko ambavyo IEBC ilinuia kutumia katika uchaguzi huo.

Kilichoibua maswali miongoni mwa maafisa hao ni kuwa walikuwa wamebeba vibandiko hivyo katika mikoba yao ya kibinafsi na hawakuandamana wala kupokelewa na ofisa yeyote wa IEBC.

Wakili Soweto pia aliuliza ni kwa nini Fomu 34A asili, ambazo zilikuwa za rangi, zilionekana katika mtandao wa IEBC zikiwa za rangi nyeupe na nyeusi.

“Fomu 34A halisi zilikuwa za rangi na ikiwa picha zao zilitumwa zilivyopigwa mbona zilionekana nyeupe na nyeusi,” alisema.

Wakili huyo pia alionyesha mahakama hiyo jinsi mitambo ya teknolojia ya KIEMs ilikuwa ikituma matokeo ya kuhitilafiana kutoka kaunti za Nyeri na Bungoma.

Lakini wakili wa IEBC, Mahat Somane alipinga madai ya Soweto akieleza kuwa sava hazikuingiliwa na hakuna ushahidi wa kuonyesha kuwa zilivurugwa.

“Mlikuwa na mawakala katika vituo vya kujumlisha kura katika maeneo Bunge, ambako kulikuwa na fomu asilia, pia mlikuwa na maajenti katika kituo cha kitaifa cha kujumlisha kura. Fomu zilizotumwa zilikuwa halisi,”

“Vile vile, haiwezeni kuwa mtambo mmoja wa KIEMs unaweza kutuma matokeo tofauti kutoka sehemu tofauti; Mlima Elgon na Nyeri. Kwa hivyo, kauli hii ni ya kubuni na haiwezi kukubalika,” alidai Somane.

Kwa upande wake, wakili Tom Ojienda alidai kuwa hakuma mgombea aliweza kupata asilimia 50 ya kura zilizopigwa, ili atangazwe mshindi katika uchaguzi wa urais.

Profesa Ojienda alikuwa akimwakilisha Seneta Mteule wa Busia Okiya Omtatah ambaye pia aliwasilisha hesabu katika mahakama hiyo kutetea msimamo huo kuwa kati ya Ruto na Odinga hamna aliyepata idadi inayotosha ya kura kutawazwa mshindi.

Wakili wa Khelef Khalifa, Willis Otieno pia aliiomba mahakama hiyo kutupilia mbali matokeo yaliyongazwa na Chebukati kutokana na mgawanyiko katika tume hiyo.

Alidai kuwa matokeo ya ukaguzi wa kura za urais kutoka maeneo 15 nchini yalionyesha dosari nyingi ambazo zinaweza kuathiri matokeo yaliyotangazwa na IEBC.

Hakikikisho la haki

Wakati huo huo, Jaji Mkuu Martha Koome amewahakikishia Wakenya kuwa yeye na wenzake watatoa uamuzi utakaozingatia Katiba na sheria.

Katika hotuba ya mwisho, Jaji huyo aliwaomba mawakili wa pande zote na Wakenya kuwaombea ili watoe uamuzi wenye “busara kubwa na unaoendeleza demokrasia”.

“Kazi ambayo, tumemaliza leo (jana Ijumaa) ndiyo ilikuwa ngumu zaidi kuliko ile kazi ambayo tunaelekea kufanya ya kuandaa uamuzi mkubwa utakaokuza misingi ya demokrasia,” akasema Koome.

Kauli yake iliungwa mkono na Naibu wake Jaji Philomena Mwilu.

Chanzo: Mwananchi