Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yatupilia mbali rufaa wafungwa shambulio la kigaidi Kenya

Hukumu Pc Data Mahakama yatupilia mbali rufaa wafungwa shambulio la kigaidi nchini Kenya

Fri, 24 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama nchini Kenya imetupilia mbali rufaa ya wanaume wawili wanaotumikia kifungo cha muda mrefu kwa kuhusika katika shambulio la chuo kikuu cha Garissa mwaka 2015, lililosababisha vifo vya watu 148.

Jaji Cecilia Githua alisema Hassan Edin Hassan na Mohammed Abdi Abikar watatumikia kifungo cha miaka 41 jela kwani rufaa yao haikuonyesha kuwa mahakama ya mahakimu ilikosea kutoa hukumu hizo ndefu.

Wakenya hao wawili walipatikana na hatia mwaka wa 2019, huku Rashid Mberesero, raia wa Tanzania, akihukumiwa kifungo cha maisha jela kabla ya kujiua mwaka 2020.

Wote walipatikana na hatia ya kula njama ya kufanya shambulizi la kigaidi na kuwa wanachama wa kundi lenye uhusiano na al-Qaeda, al-Shabab, lakini walikata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama ya mahakimu.

Lakini katika uamuzi wake, jaji wa mahakama kuu alisema adhabu hiyo ni ndogo kwa kuzingatia "vitendo viovu, vilivyopangwa kimakusudi vilivyosababisha mateso mengi kwa familia za wahasiriwa" Wawili hao wanaweza kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo katika Mahakama ya Rufaa ndani ya wiki mbili.

Shambulio hilo katika chuo kikuu hicho ambalo liliwauwa hasa wanafunzi, lilikuwa shambulio la pili kwa mauti zaidi kufanywa na kundi hilo nchini Kenya.

Shambulio la al-Qaeda katika ubalozi wa Marekani mwaka 1998 liliua zaidi ya watu 200.

Kesi hii imekuwa ya muda mrefu na imeahirishwa mara kadhaa tangu wafungwa hao kukamatwa mara tu baada ya shambulio la Aprili 2015 katika chuo kikuu.

Na leo haikuwa tofauti, mahakama ilitatizwa kwa muda huku hakimu akitoa uamuzi wake kupitia njia ya video, baada ya muunganisho wake kupotea.

Wafungwa hao ambao walikuwa wakisikiliza hukumu hiyo kimyakimya kutoka gerezani, walizungumza kwa muda mfupi huku mahakama ikisubiri hakimu arudi mtandaoni

Chanzo: www.tanzaniaweb.live