Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama yamnyima dhamana waziri mkuu wa zamani wa Burundi

Mahakama Yamnyima Dhamana Waziri Mkuu Wa Zamani Wa Burundi Mahakama yamnyima dhamana waziri mkuu wa zamani wa Burundi

Fri, 6 Oct 2023 Chanzo: Bbc

Mahakama nchini Burundi imemnyima dhamana waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo Alain-Guillaume Bunyoni, ambaye ameshtakiwa kwa shutuma za kuhujumu usalama wa taifa na kumtusi rais, vyanzo karibu na kesi hiyo vililiambia shirika la habari la AFP siku ya Alhamisi.

Bunyoni alikuwa waziri mkuu kuanzia katikati ya mwaka 2020 lakini aliachishwa kazi kutokana na mzozo wa ngazi ya juu wa kisiasa mwezi Septemba mwaka 2022, siku chache baada ya Rais Evariste Ndayishimiye kuonya kuhusu njama ya "mapinduzi" dhidi yake.

Mkuu huyo wa zamani wa polisi na waziri wa usalama wa ndani, Bunyoni alikuwa akionekana kama mkuu wa baraza la viongozi la kijeshi linalojulikana kama "majenerali" wenye nguvu ya kweli ya kisiasa nchini Burundi.

Alikamatwa Aprili mwaka huu katika mji mkuu wa kiuchumi wa Burundi Bujumbura usiku wa kuamkia sikukuu yake ya kuzaliwa akitimiza miaka 51, na amezuiliwa katika mji mkuu wa kisiasa wa Gitega.

Kesi hiyo ilianza mwishoni mwa mwezi uliopita katika kesi iliyoendeshwa na mahakama ya juu huko gerezani. "Mahakama ya Juu ilitoa uamuzi wake siku ya Jumatatu, na kuamua kukataa ombi la Jenerali Bunyoni ili kuachiliwa kwa muda," chanzo cha mahakama kililiambia shirika ka habari la AFP kwa sharti la kutotajwa jina, na kuongeza kuwa alifahamishwa kuhusu uamuzi huo siku ya Jumatano. Chanzo cha gereza kilithibitisha habari hiyo.

Mbali na kukabiliwa na mashtaka ya "kuhujumu usalama wa ndani ya nchi, kuhujumu utendakazi mzuri wa uchumi wa taifa na kujitajirisha kinyume cha sheria", Bunyoni pia anatuhumiwa kumiliki silaha kinyume cha sheria na kumtukana rais.

Bunyoni alikuwa mshirika wa karibu wa rais wa zamani Pierre Nkurunziza, alikuwa kiongozi mwenye ushawishi mkubwa katika chama tawala cha CNDD-FDD.

Chanzo: Bbc