Mahakama ya kijeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Imekataa jaribio la kumfanya Rais wa zamani Joseph Kabila kuwa shahidi katika kesi ya mauaji ya mwanaharakati maarufu wa haki za binadamu, Floribert Chebeya.
Askari watatu wa polisi walikata rufaa dhidi ya adhabu ya kifo kuhusiana na mauaji ya Chebeya mwaka 2010 - katika tukio lililozusha wasiwasi wa kimataifa kuhusu ukiukaji wa haki binadamu wakati wa utawala wa Kabila.
Mkuu wa mahakama Kuu Kanali Ekofo aliwashangaza waliokuwepo alipokumbusha kuwa sheria inampa uwezo wa hiari kutoa mtazamo wake katika aina hiyo ya uamuzi lakini pia alionyesha kuwa kuna kasoro ya utaratibu katika mbinu za upande wa mashtaka. Bila kutoa maelezo zaidi juu ya sababu za uamuzi wake huo alikitaja kifungu cha 249 cha sheria ya mahakama ya kijeshi ambacho kinampa mamlaka ya hiari ya kuamua kuletwa mbele ya mahakama kwa mtu fulani aliyetajwa au la. Lakini kwa upande wa Rais Mstaafu Joseph Kabila hakukua na tamko lolote. Walalamikaji wa kiraia katika kesi hiyo pamoja na mashirika 50 yasio ya kiserikali, walikuwa wameiomba mahakama kumleta Kabila na watu wengine kadhaa kutoa ushahidi, lakini ombi lilikataliwa.
Chebeya alikutwa amekufa katika gari yake nje kidogo ya mji mkuu wa Kinshasa Juni 2010. Alikuwa ameitwa kituo cha polisi siku iliyotangulia ambako alipelekwa na dereva wake, ambaye pia alitoweka na anashukiwa kuwa ameuawa.
Waendesha mashtaka wa kijeshi walisema hivi karibuni kwamba wanashuku mkuu wa zamani wa polisi wa taifa hilo, Jenerali John Numbi, pia alitoa mchango katika mauaji hayo. Numbi ametoweka tangu wakati huo.