Mahakama ya Nigeria imeamuru kuchinjwa kwa jogoo siku ya Ijumaa baada ya malalamiko ya majirani kuhusu kuharibu mazingira kwa kelele, vyombo vya habari vya nchini humo vimeripoti.
Mahakama katika mji wa kaskazini wa Kano ilitangaza jogoo kuwa kero kwa mtaa huo baada ya kuwika mara kwa mara ambapo majirani wawili walisema kuwa kuliwanyima usingizi, ripoti ya tovuti ya Premium Times.
Mmoja wa majirani hao, Yusuf Muhammed, aliiambia mahakama kuwa kuwika kwa jogoo bila kuchoka ni kukiuka haki yake ya kupata usingizi mwanana.
Isyaku Shu'aibu aliambia mahakama kwamba alinunua kuku huyo kwa ajili ya sherehe za Ijumaa Kuu na akaomba apewe hadi siku kuu ya Kikristo kabla ya kumuua kwa ajili ya karamu ya familia.
Hakimu Halima Wali alikubali ombi hilo Jumanne lakini akamuonya kuzuia jogoo huyo kuzurura eneo hilo na kuwasumbua wakaazi, tovuti ya habari ya Daily Trust inaongeza.
Mmiliki huyo pia aliamriwa kuhakikisha anamchinja kuku huyo siku ya Ijumaa kama alivyoahidi au atakabiliwa na adhabu.