Mahakama kuu nchini Kenya imetaja kutumwa kwa maafisa wa polisi nchini Haiti kuwa ni kinyume cha sheria.
Jaji huyo alisema Baraza la Usalama la Kitaifa, linalomjumuisha Rais, halina mamlaka ya kupeleka polisi wa kawaida nje ya nchi.
Aliongeza kuwa baraza hilo linaweza tu kupeleka vikosi vya kijeshi ambavyo ni pamoja na jeshi la nchi kavu , jeshi la anga na jeshi la wanamaji kwa misheni kama hiyo ya kulinda amani kama vileya nchini Haiti.
Ekuru Aukot, kiongozi wa upinzani aliyewasilisha ombi kwa kesi hiyo, alisema huu ulikuwa ushindi kwa Kenya na kwamba nchi haiwezi kumudu kuwaachilia maafisa kabla ya kukabiliana na changamoto zake za usalama.
Aukot aliongeza kuwa Rais William Ruto alikuwa akitumia tu kikosi hicho kuimarisha hadhi yake ya kimataifa na kutafuta kupendwa namataifa ya magharibi kama vile Marekani.
Kabla ya uamuzi huo, afisa wa polisi ambaye alizungumza na BBC bila kutajwa jina, alisema kuwa walikuwa wamepokea miezi miwili ya mafunzo ya kina.
Mnamo Septemba 2023, Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry alihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa akitoa wito wa kutumwa kwa haraka kwa kikosi cha kimataifa.
Alisema serikali yake imezidiwa nguvu na magenge ambayo yanadhibiti asilimia 80 ya mji mkuu wa Port-au-Prince.
Kenya ilijitolea kuongoza kikosi cha kimataifa na kuahidi kutuma maafisa kwa idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Rais William Ruto alisema Kenya ina ‘rekodi ya kuvutia’ ya ushiriki katika usaidizi wa amani kote ulimwenguni.
Aliongeza kuwa kutumwa huko kutawawezesha maafisa kuboresha na kuimarisha ustadi wao, ujuzi na uzoefu katika kutoa usalama.
Serikali kupitia msemaji wake Isaac Mwaura imesema itakata rufaa dhidi ya uamuzi huo.Mwaura kupitia taarifa kwa vyombo vya habari amesema Kenya inaheshimika kwa mchango wake wa kuwatuma walinda usalama wake kwa misheni za kudumisha amani kote duniani na itapigania haki ya kufanya hivyo.