Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama kuchunguza mpango wa Katumbi kuwania Urais

Moses Katumbi.jpeg Mahakama kuchunguza mpango wa Katumbi kuwania Urais

Sat, 28 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama ya Katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imechunguza siku ya Ijumaa mizozo ya wagombea katika uchaguzi wa rais wa Desemba 20, ikiwa ni pamoja na ombi la kupinga uraia wa mwanasiasa wa upinzani Moïse Katumbi, amebainisha mwandishi wa habari wa shirika la habari la AFP

Hivi karibuni Tume ya uchaguzi (CENI) ilitangaza kuruhusiwa kwa wagombea 24 waliosajiliwa kwa uchaguzi huu mkuu na kuchapisha orodha ya muda mnamo Oktoba 20. Tangu wakati huo, maombi ya kupinga baadhi ya wagombea yamewasilishwa katika Mahakama ya Kikatiba.

Miongoni mwa waliotuma maombi, Noël Tshiani, pia mgombea urais, anaomba kufutwa jina la Moïse Katumbi miongoni mwa wagombea urais kutokana na kuwa "sio raia wa Kongo".

Noël Tshiani ndiye muanzilishi wa dhana ya "baba na mama", sheria inayopendekezwa kuhusu uraia wa Kongo, ambayo inalenga kukubali katika nyadhifa za juu tu Wakongo waliozaliwa na wazazi wawili wenye uraia wa Kongo. Njia ya kumuondoa kwenye kinyang'anyiro hicho Moïse Katumbi hasa, ambaye baba yake alikuwa Mwitaliano.

Wakati wa mjadala huo, Bw. Tshiani amethibitisha kwamba Bw. Katumbi, mfanyabiashara tajiri na gavana wa zamani wa Katanga, "ni raia wa Italia."

Amewasilisha kifungu kwa vyombo vya habari ili kuhalalisha ombi lake lakini "hakutoa uamuzi wa mamlaka ya Italia unaotambua uraia huu kwa Moïse Katumbi, wala uamuzi wowote wa mamlaka ya kigeni unaompa Moïse Katumbi uraia mwingine isipokuwa uraia wa Kongo", amejibu wakili Hervé Diakiese, mwanasheria wa Moïse Katumbi.

Ofisi ya mwendesha mashtaka wa umma haikutoa maoni yake wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo lakini ilmebaini kwamba itaiandika kwa maandishi uamuzi wake kufikia Jumatatu.

Katika ombi jingine, Seth Kikuni, ambaye pia ni mgombea urais, ametoa wito wa kufutwa kwa ugombea wa rais anayemaliza muda wake Félix Tshisekedi, ambaye anawania muhula mpya wa miaka mitano, kwa misingi kwamba rais huyo aliongeza jina la kwanza Antoine katika utambulisho wake. Akiwa madarakani tangu Januari 2019, Bw. Tshisekedi ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kushinda katika uchaguzi huu wa duru moja.

Uamuzi wa mahakama unatarajiwa Jumatatu, Oktoba 30, wakati orodha ya mwisho ya wagombea itachapishwa Novemba 18, mkesha wa ufunguzi rasmi wa kampeni za uchaguzi.

Uchaguzi wa urais utaambatana na uchaguzi wa wabunge, wa magavana na serikali za mitaa, ambapo maelfu ya wagombea wamesajiliwa.

Hali ya kisiasa imekuwa ya sintofahamu kwa miezi kadhaa, huku vyama vya upinzani vikishutumu kupungua kwa nafasi ya kidemokrasia na kusema vina imani kuwa uchaguzi huo utagubikwa na udanganyifu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live