Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Magufuli asamehe Waethiopia 1,789

27c19a88e54bbedfec1776911227f1dc Magufuli asamehe Waethiopia 1,789

Tue, 26 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

TANZANIA na Ethiopia zimekubaliana kushirikiana katika maeneo mapya ikiwemo majeshi, biashara na uwekezaji kwa lengo la kukuza zaidi uchumi.

Aidha, Tanzania imeahidi kuwaachia wafungwa wa makosa ya uhamiaji haramu raia wa Ethiopia 1,789 bila masharti na imeiomba nchi hiyo iifundishe Tanzania namna ya kutumia sekta ya mifugo kwa manufaa ya kiuchumi.

Hayo yamebainishwa na marais wa Tanzania, Dk John Magufuli na wa Ethiopia, Sahle-Work Zewde katika mkutano wao na waandishi wa habari wakati wa ziara ya siku moja ya Rais huyo wa Ethiopia jana wilayani Chato mkoani Geita.

Rais Magufuli alisema kwa sasa nchi hizo zinaendelea na majadiliano kuhusu ushirikiano wa majeshi na ufundishwaji wa Lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Addis Ababa.

Alisema Ethiopia ni nchi ambayo uchumi wake uko juu na huenda ndio inayoongoza kwa uchumi Afrika, ambapo mwaka jana uchumi wake ulikuwa unakua kwa asilimia tisa.

Aidha, alisema nchi hiyo inaongoza kwa kuwa na mifugo mingi Afrika wakati Tanzania ni ya pili. “Wenzetu wamefaidika sana na sekta ya mifugo sisi hatujanufaika. Wao wanatengeneza mabegi, mikanda na viatu yenye soko kubwa Ulaya. Nimezungumza na rais na kumuomba kukaribisha wawekezaji lakini pia kuangalia ni namna gani ya kujifunza kwao ili kuendeleza sekta hiyo,” alisema Rais Magufuli.

Aidha, alisema katika mazungumzo yake na Rais huyo wa Ethiopia walikubaliana kuwa mazungumzo ya Tume ya Pamoja baina ya nchi hizo mbili yafanyike chini ya mawaziri husika kati ya Machi na Aprili mwaka huu. Alisema Tanzania na Ethiopia zina uhusiano mzuri ulioanza tangu wakati wa kuanzishwa kwa Umoja wa Nchi za Afrika (OAU) na harakati za ukombozi wa bara la Afrika.

“Waasisi wa mataifa yetu Mwalimu Julius Nyerere na hayati Mfalme Haile Sellasie walikuwa mstari wa mbele katika uanzishwaji wa OAU na harakati za ukombozi mwaka 1963. Tumeendelea na ushiano huo mkubwa ulionufaisha nchi zetu katoka nyanja mbalimbali,” alisema Rais Magufuli.

Alieleza namna biashara baina ya Tanzania na Ethiopia inavyokua ambapo mwaka 2016 biashara ilikuwa Sh bilioni 3.07, lakini mwaka 2019/20 imefikia Sh bilioni 13.55. Na katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajili miradi 13 kutoka Ethiopia yenye thamani ya dola za Marekani milioni 14.57 na kutoa ajira zipatazo 677.

Alisema pamoja na biashara, pia nchi hizo zinashirikiana katika usafiri wa anga na utalii, ambako Shirika la Ndege la Ethiopia linafanya safari zake kwenye viwanja vya ndege vitatu nchini; Dar es Salaam, Kilimanjaro na Zanzibar.

“Lakini pia Watanzania wamekuwa wakipata fursa ya masomo nchini Ethiopia ambapo jumla ya marubani 75 na wahandisi wa ndege 20 wanasoma Ethiopia,” alisema Rais Magufuli.

Alisema pia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na Shirika la Ndege Ethiopia wameingia kwenye makubaliano ya matangazo kwa ajili ya kusaidia kuongeza idadi ya watalii. Kuhusu wafungwa ambao ni wahamiaji haramu kutoka Ethiopia, Rais Magufuli alisema kwa sasa wapo wafungwa wapatao 1,789 kutoka Ethiopia wanaoingia nchini pasipo uhalali na wamehukumiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Alisema amezungumza na Rais Zewde juu ya namna ya kuwaruhusu wafungwa hao warejee kwao huku akisisitiza kuwa wataruhusiwa bila masharti yoyote baada ya kuzingatia undugu na urafiki uliopo baina ya nchi hizo mbili.

“Nimemueleza rais wana ndege wakichukua Dreamliner inayobeba watu 260 wakipiga trip (safari) tano na Airbus moja maana yake hawa wakimbizi wote watarudi kwao na watawatumia vizuri kujenga uchumi wa Ethiopia. Amekubali na amesema akirudi nyumbani watalijadili,” alifafanua.

Pamoja na hayo, alisema wamezungumzia suala la kurejeshewa kiwanja cha kujenga ubalozi jijini Addis Ababa ambacho cha awali kilichukuliwa na Serikali ya Ethiopia kutokana na kutoendelezwa kwa mujibu wa sheria.

“Uwanja wetu kule Ethiopia tuliochelewa kuujenga kwa sababu hela tulizopeleka kule zililiwa na balozi wetu na kiwanja tukakirudisha kwa kushindwa kutimiza masharti tumemuomba aturudishie na tumemuahidi tutakiendeleza kwa kujenga,” alisema Rais Magufuli.

Alisema Serikali ya Tanzania pia imeipatia Ethiopia ekari tano jijini Dodoma kujenga majengo ya ubalozi wake. Kwa upande wake, Rais wa Ethiopia alisema wamekubaliana kushirikiana katika maeneo mapya zaidi ikiwemo uwekezaji na biashara, na nchi yake iko tayari kushirikiana katika maeneo hayo ili kukuza uchumi wa nchi zote mbili.

“Tanzania ni nchi muhimu kabisa si tu Afrika Mashariki ila Afrika nzima, kwetu sisi inaunganisha Pembe ya Afrika hadi Kusini mwa Bara la Afrika,” alibainisha.

Alieleza kuwa nchi yake inataka kuwa na uhusiano wenye mizizi imara na Tanzania ndio maana jukumu la kwanza la Tume ya Ushirikiano itakuwa ni kupitia mikataba iliyopo na kuangalia maeneo mengine mapya ya ushirikiano.

Alisema kati ya mambo aliyokubaliana katika mazungumzo yake na Rais Magufuli ni kushirikiana katika biashara na uweekzaji kwa sababu anaamini Afrika inaweza kuwekeza katika nchi za Afrika na si kusubiri wageni waje wawekeze.

Kuhusu sekta ya mifugo, alisema nchi yake itatoa kipaumbele katika sekta hiyo kutokana na ukweli kuwa Tanzania na Ethiopia ndio nchi zinazoongoza kwa mifugo Afrika. Akizungumzia wahamiaji haramu, Rais Zewde alisema amezingatia ombi la Rais Magufuli na kumshukuru kwa kuwaruhusu wafungwa hao kuondoka bila masharti yoyote na kuahidi kufanya kila awezalo kutekeleza ombi hilo kupitia Ubalozi wa Ethiopia ulipo nchini.

Kuhusu kiwanja cha Addis Ababa cha ujenzi wa Ubalozi wa Tanzania, alibainisha kuwa nchi yake iko kwenye mpango wa kuhakikisha nchi zote za Afrika zinakuwa na balozi zao jijini humo ambako ndio pia makao makuu ya Afrika.

“Tunafurahi pendekezo lako la Kiswahili kufundishwa katika Chuo Kikuu cha Addis Ababa kwa sababu Ethiopia ni nchi yenye makabila mengi na hasa ikizingatiwa kuwa Kiswahili ni moja ya lugha inayotumika zaidi Afrika,” alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz