Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Magufuli alikuwa ‘mfanyakazi  namba moja’ wa bandari zetu

C9f082bf36d7c6c479129f3c9ac6518d Magufuli alikuwa ‘mfanyakazi  namba moja’ wa bandari zetu

Tue, 23 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko, alikuwa akimshukuru na kujivunia sana aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli, kutokana na kampeni zake alizokuwa anafanya kwa ajili ya kunyanyua bandari za Tanzania.

“Hakuna kampeni kubwa ya biashara (kwa ajili ya bandari zetu) kuliko anayotufanyia yeye (Magufuli). Sisi tunamwita mfanyakazi namba moja wa bandari. Anapofanya mahusiano na viongozi wenzake wa nchi jirani, wanakuja nchini mwetu, na wengi wametembelea bandari, hapo anakuwa ametupa msingi,” alisema Kakoko alipofanya mahojiano na gazeti hili wakati wa uhai wa Dk Magufuli.

Oktoba, 2016 Magufuli alimkaribisha nchini aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Joseph Kabila na baada ya kufanya naye mazungumzo na kisha akaweka jiwe la msingi la jengo la TPA.

Yote hayo yalilenga katika kuvutia wafanyabiashara wa nchi hiyo kuongezea bidhaa zao wanazopitishia katika Bandari ya Dar es Salaam.

Kama hiyo haitoshi, wakati Rais Felix Tshisekedi aliyempokea kijiti Kabila alipotembelea Tanzania Juni, 2019, Rais Magufuli pia alihakikisha anatembelea bandari ya Dar es Salaam katika harakati zile zile za kujenga uhusiano mzuri ili kuhakikisha bandari ya Dar es Salaam inanufaika na shehena inayokwenda au kutoka DRC.

Desemba 2016, Rais Magufuli pia alimkaribisha nyumbani Rais wa Zambia, Edger Lungu na kama kawaida hakusita kumpangia mgeni wake kutembelea Bandari ya Dar es Salaam katika muktadha huo huo wa kujenga uhusiano mzuri baina ya Zambia na Tanzania, mintarafu suala zima la mzigo wa Zambia kupitia Dar es Salaam.

Marais wengine waliotembelea Tanzania huku suala la nchi zao kutumia zaidi Bandari ya Dar es Salaam ikiwa ni moja ya ajenda ni marais wa Rwanda, Uganda, Malawi na Sudan Kusini.

Septemba mwaka jana, Magufuli na Rais Evarist Ndayishimiye wa Burundi walifanya mkutano mkoani Kigoma na kuamua kufanya ushirikiano zaidi wa kidiplomasia na kiuchumi ikiwa ni pamoja na namna ya kushirikiana katika suala la bandari.

Hatua hiyo imesababisha Tume ya Kudumu ya Pamoja (JPC) baina ya serikali ya Tanzania na Burundi kukutana hivi karibuni mjini Kigoma katika harakati za kutekeleza ushirikiano huo.

Mkutano huo ulioshirikisha mawaziri wa mambo ya nje wa Tanzania, Palamagamba Kabudi na mwenziye wa Burundi, Albert Shingiro, ulienda sambamba na viongozi hao kutembelea miradi ya kimkakati ya kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na uchumi ikiwemo mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu ya jua uliopo eneo la ukanda maalumu wa kiuchumi (KISEZ) katika Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Sambamba na mradi huo, viongozi hao pia walitembelea upanuzi na uboreshaji wa uwanja wa ndege wa Kigoma, mradi wa ujenzi wa bandari Kavu Katosho mjini Kigoma, bandari ya Kigoma na pia wakatembelea eneo ambalo kutajengwa forodha ya pamoja katika eneo Manyovu wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma na Mugina mkoani Makamba nchini Burundi.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Kakoko, aliwaleza viongozi hao kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la shehena inayokwenda Burundi kupitia bandari ya Kigoma.

Kakoko alisema kuwa usafirishaji huo wa shehena utaongezeka maradufu baada ya kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa bandari Kavu unaolenga kurahisisha usafirishaji mizigo kwenda mikoa ya Burundi ambayo haipakani na ziwa na ni rahisi kufikiwa na gari kutoka mkoani Kigoma.

Alisema maboresho ya bandari ya Kigoma kwa kuwekewa vifaa vya kisasa kutaongeza ufanisi wa usafirisahi wa shehena baina ya nchi hizo mbili. Burundi inasafirisha takriban asilimia 90 ya bidhaa zake kupitia Bandari ya Dar es Salaama.

Kakoko amekuwa akisema kwamba baada ya juhudi zilizokuwa zikifanywa na hayati Magufuli, kilichokuwa kinafuata ni wizara husika na watendaji wenyewe wa TPA kwenda katika nchi husika kuweka mambo sawa.

Katika hatua hiyo Kakoko anasema yeye binafsi aliwahi kwenda na kukutana ana kwa ana na aliyekuwa Rais wa Burundi, Hayati Pierre Nkrunziza.

Alisema baada ya kukutana naye kukawa na ongezeko kubwa la shehena ya Burundi inayopitia nchini mwetu.

Alifafanua kwamba kwa kawaida mzigo wa nchi hiyo huko nyuma ulikuwa wastani wa tani laki tatu na nusu, lakini mzigo wa Burundi uliongezeka na wakati anazungumza na gazeti hili tani zilikuwa zimeshafika laki nne huku zikiendelea kupanda.

“Kwa kweli idadi ya tani za mizigo zinazopotia nchini mwetu zinaongezeka kwa sababu ya kampeni ya Mheshimiwa Rais John Magufuli,” alisema Kakoko.

Jambo ambalo Watanzania wanapaswa kujua ni kwamba miradi inayotoa ajira kama ujenzi wa reli ya kisasa, madaraja ya juu, daraja la Busisi na mradi wa umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere inaongeza ajira na kukuza biashara lakini kuongezeka kwa shehena bandarini pia kunapanua biashara.

Hii ni kwa sababu shehena inapoongezeka katika bandari zetu, mbali na ujenzi ambao umekuwa ukiendelea, faida zake haziishii kwa pato linaloingia serikalini peke bali pia mawakala wa shehena hupata ajira, wasafirishaji wa mizigo hadi makuli na mama ntiliye kote ambako shehena hizo hupita hufaidika.

Kakoko pia anaipongeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kufanya kazi nzuri katika kutangaza bandari za Tanzania.

“Kwa hiyo utaona tunafanya mahusiano, siyo tu na wafanyabiashara wa nchi zinazozunguka bandari zetu, bali pia na serikali zenyewe za nchi hizo,” alisema.

Kingine wanachokifanya katika kupanua soko lao, Mhandisi Kakoko alisema ni kuboresha huduma zao.

Alisema katika kuhakikisha mteja wao anahudumiwa ipasavyo, TPA imetengeneza mkataba wa maelewano na mteja (customer chart).

Alisema wanatumia pia mitandao ya kijamii katika kuwasiliana kujua changamoto hata ndogo ndogo na kuzifanyia kazi.

“Kwa mfano, tumefungua kundi la WhatSapp ili kuelezana mambo mbalimbali ya kuboresha huduma zetu na changamoto za kila siku. Hayo yote ni katika kuboresha utendaji wetu na hivyo kuvutia masoko yetu,” alisema.

Alisema katika kuimarisha soko wamekuwa pia wakiimarisha mawasiliano na wadau ambao wanatumia bandari zetu kwa sasa.

“Tunakutana nao, tunafanya nao mikutano, tunajua namna wanavyofanya biashara na vikwazo vilivyopo na kuvitafutia ufumbuzi mara moja,” alisema.

Alisema katika suala la kutafuta masoko, TPA pia inashirikiana na sekta binafsi kama vile Chama cha Mawakala wa Shehena (TAFFA).

“Hawa TAFFA wako makini katika hili kwa sababu na wenyewe wanapata mapato yao kulingana na ukubwa (wingi) wa shehena na hivyo tunasaidiana nao kutafuta masoko,” alisema.

Alisema pia wanashiriki katika maonesho mbalimbali ya biashara yanayofanyika katika nchi za wadau ili kujitangaza zaidi. Alisema takribani nchi zote za wadau wanaopitishia mizigo yao Tanzania (Uganda, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi, Zambia na Malawi n.k), wamefanya maonesho yao huko.

“Tumeshashiriki kwenye hizo nchi zote za wadau katika maonesho yao ya kibiashara ya kimataifa. Sehemu nyingine tumepata hadi vyeti vya zawadi,” alisema na kutaja moja ya nchi waliopata tuzo kuwa Uganda na kwamba tuzo hiyo walipewa na wafanyabiashara wa Kampala.

Lingine wanalofanya TPA ili kukuza masoko kwa mujibu wa Mhandisi Kakoko ni kutembelea maeneo wanayodhani wanaweza kuongeza soko lao na kisha kufanya mikutano na wahusika.

Alifafanua kwamba huko wanaangalia viwanda, maduka, waagizaji wa mafuta na kila aina ya uzalishaji na kufanya nao mazungumzo kuhusu wanavyoweza kunufaika na kupitishia mizigo yao katika bandari za Tanzania.

“Kwa mfano tumekwenda hadi Kitwe na Mufulira nchini Zambia kuongea nao,” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz