Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Magazeti Alhamisi, Oktoba 28: Waiguru katika hatari ya kukamatwa kwa ufisadi

18f914c88a424118 Magazeti Alhamisi, Oktoba 28: Waiguru katika hatari ya kukamatwa kwa ufisadi

Thu, 28 Oct 2021 Chanzo: kiswahili.tuko.co.ke

Magazeti ya Alhamisi, Oktoba 28, yameipa uzito kesi ya Mbunge wa Kapseret, Oscar Sudi ambapo anatuhumiwa kughushi vyeti vyake vya masomo.

Magazeti haya pia yameguzia athari za hatua ya gavana wa Kirinyaga, Anne Waiguru kujiunga na chama cha Naibu Rais William Ruto, United Democratic Alliance (UDA).

1. The Standard Gazeti hili linaripoti kuwa mahakama moja jijini Nairobi iliambiwa Jumatano, Oktoba 27, kuwa Mbunge Oscar Sudi alighushi vyeti vyake kuwania kiti katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2013.

Mashahidi wawili walisema mbunge huyo hakufanya mtihani wa KCSE wala kufuzu na diploma katika Masuala ya Usimamizi wa Sekta ya Utalii na vyeti hivyo ni vya watu wengine.

Sudi, 41, amepitia maisha magumu kabla ya kuwa mtu maarufu akikulia katika familia ya ufukara.

Alianza kama mchungaji wa mifugo, kisha alipanda ngazi na kuwa muuzaji wa makaa na mboga, kisha kondakta wa matatu kabla ya kujinunulia gari lake la kubeba abiria.

Katika mahojiano, Sudi alisema alizaliwa mwaka 1980 karibu na Chuo Kikuu cha Moi, Kesses na walikuwa wanaishi katika nyumba ya nyasi kama maskwota kwenye shamba la Talai.

Alisema uhaba wa karo ulimchochea kufanya kazi za sulubu kupata mkate.

Huku akikumbana na vizingiti, alipata umaarufu na kuchaguliwa kuwa mbunge wa Kapseret kupitia chama cha United Republican(URP) mwaka 2013.

2. Daily Nation Daily Nation linaripoti kuwa kinara wa ODM Raila Odinga ameahirisha kampeni zake za "Azimio la Umoja" nchini kwa wiki mbili kuhudhuria kongamano la miundombinu katika Taifa la Milki ya Uarabuni.

Kinara huyo wa upinzani na majemedari wake waliondoka nchini Jumatano, Oktoba 27.

Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed ni miongoni mwa maafisa walioandamana na Raila kwa kongamano hilo nchini Dubai.

Raila anatarajiwa kuarifu kongamano hilo kuhusu faida ya kuendelea kuwashirikisha washikadau kama njia bora ya kubuni muundo msingi ulimwenguni.

3. The Star

Gazeti hili linaripoti kuwa Gavana Waiguru amesisitiza kuwa Ruto ndiye atakuwa rais mpya wa Kenya.

Katika mahojiano na gazeti hili,Waiguru alisema ishara zote zinaonyesha kuwa Ruto ndiye atakuwa rais na ana uwezo kwa kustawisha uchumi wa taifa hili.

Waziri huyo wa zamani wa Ugatuzi alisema kati ya wagombeaji wa urais ambao wametangaza azma yao ya kuingia Ikulu, ni Ruto pekee ambaye anaweza kuendeleza kile serikali ya Jubilee na kaunti zimeweza kutimiza.

Mkosoaji huyo wa zamani wa Ruto na mtetezi wa handsheki alisema kuwa hajutii akidai kuwa kupitia siasa za BBI hakuwa na uhasama wowote na naibu rais.

4. Taifa LeoTaifa Leo linaripoti kuwa wahudumu 290 wa afya kati ya 300 ambao walichaguliwa kwa kazi ya Uingereza walifeli mtihani wa Kingereza.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe aliwataka wahudumu hao kuboresha Kizungu chao ili kupata kazi za ughaibuni.

Kagwe alisema inasikitisha kuwa wafanyakazi hao walifuzu kwa kazi hiyo ya Uingereza lakini walikataliwa sababu ya lugha.

Aliomba taasisi za utabibu kufunza kozi ambazo zitawasaidia kupota kazi nje ya nchi.

5. People Daily Gazeti hili linaripoti kuwa huku Waiguru akihamia katika kambi ya Ruto, makachero wanakamilisha uchunguzi kuhusu tuhuma za ufisadi dhidi yake ambapo huenda atakamatwa mapema wiki ijayo.

Pia wengine ambao huenda watashtakiwa pamoja na Waiguru ni Afisa Mkuu wa Fedha za Kaunti Mugo Ndathi, Spika wa kaunti ya Kirinyaga Anthony Gathumbu, Kiongozi wa Wengi James Murango na mwenyekiti wa kamati ya bajeti David Mathenge.

Sadfa ni kwamba wanne hao waliandamana na gavana huyo katika makazi ya Ruto mtaani Karen na kuhamia rasmi katika chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Chanzo: kiswahili.tuko.co.ke