Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Magavana wa Benki wamaliza mkutano Burundi na maazimio

A6b7d900e208233a002b86c308823cce.jpeg Magavana wa Benki wamaliza mkutano Burundi na maazimio

Sun, 8 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUTANO wa 58 wa Magavana wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF) kutoka nchi 54 za Bara la Afrika umemalizika mjini Bujumbura, Burundi kwa kutoa maazimio, ikiwamo kuziomba taasisi za fedha za kimataifa zijenge uwezo wa miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika nchi za Afrika kwa ajili ya kuchochea uchumi wa nchi hizo.

Maazimio mengine ya magavana hao ni kuyaomba mashirika hayo ya fedha ya kimataifa kuzipatia nchi zao rasilimali fedha kwa ajili ya kukabiliana na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia hususan katika suala la biashara ya mtandao, uchumi wa kidijitali na ujenzi wa miundombuni ya kidijitali ili kuifikia sehemu kubwa ya wananchi mijini na vijijini

Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Yussuf Masauni alisema jana kuwa, msimamo huo wa pamoja umelenga kuwawezesha wananchi kuwa na uwezo wa kutumia teknolojia ya kidijitali katika kufanya shughuli zao za kiuchumi na kijamii hususan katika kipindi hiki cha changamoto ya ugonjwa wa covid-19.

“Kizazi kilichoelimika kuhusu matumizi ya kidijitali kinachangia maendeleo na kubuni nyenzo zinazosaidia kutekeleza kazi za ubunifu ili kukuza ajira na kuboresha maisha ya wananchi,” alisema Masauni.

Alizungumzia pia suala la umuhimu wa nchi za Afrika zenye vyanzo vya uhakika vya nishati ya umeme kujengewa uwezo na Benki ya Dunia na IMF ziweze kufua umeme kutokana na kuwa na vyanzo vya gharama nafuu kama maji na gesi asilia pamoja na kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi wengi ili kuwezesha upatikanaji wa huduma za kidijitali.

“Takwimu zinaonesha idadi ya watu wanaopata huduma ya nishati ya umeme Barani Afrika imefikia chini ya asilimia mbili, hivyo kuna umuhimu mkubwa wa taasisi hizo za fedha duniani kuzipatia nchi za Afrika rasilimali fedha kwa ajili ya miradi hiyo,” alisema Masauni.

Alisema pia kutokana na changamoto kadhaa ikiwamo za umeme na miundombinu ya kidijitali, robo tatu ya wakazi bilioni 1.3 barani Afrika hawatumii intaneti, jambo linalokwaza kutumia fursa za kidijitali katika kuendesha maisha yao.

“Katika suala la umeme Tanzania tumepiga hatua kubwa ya usambazaji wa umeme vijijini kupitia mradi wa Rrea, lakini tunahitaji fedha zaidi kwa ajili ya kutekeleza miradi itakayochochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu katika nyanja ya matumizi ya dijitali, sekta ambayo hivi sasa ina ajiri idadi kubwa ya watu wakiwemo vijana na ni lazima miradi hiyo iwe ni ile yenye tija,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayesimamia nchi za Afrika, Dk Taufila Nyamadzabo alisema mkutano huo ulikuwa na mafanikio makubwa na kuahidi kuwa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani zitayafanyiakazi kikamilifu maazimio yaliyofikiwa wakati wa mikutano ya taasisi hizo iliyopangwa kufanyika Oktoba, mwaka huu, Washington, Marekani

“Kimsingi naamini Benki ya Dunia na IMF zitatoa fedha kwa nchi za Afrika katika kutimiza malengo yao ya kuwa na uwezo wa matumizi ya mifumo ya kidijiti, mifumo ya biashara ya mtandao pamoja na kuboresha nishati ya umeme, lakini fedha hizo zitatolewa kwa kila nchi kivyake kadri zitakavyoomba kulingana na mahitaji na vigezo vinavyotakiwa,” alisema Dk Nyamadzabo

Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Dk Jilly Maleko alisema mkutano huo umefanyika muda muafaka kwa ajili ya mustakabali wa nchi za Afrika ambazo zimeathiriwa kwa kiasi kikubwa kiuchumi kutokana na kusimama kwa shughuli nyingi za uzalishaji kwa sababu ya ugonjwa wa covid-19.

“Wito wangu kwa Watanzania hasa vijana ni kuchangamkia fursa zitakazopatikana baada ya makubaliano yaliyofikiwa hapa kwa sababu katika kipindi hiki mifumo ya kidijitali kwa kutumia simu na kompyuta ndiyo inayotumika kwa kasi katika fursa mbalimbali za kujiletea maendeleo hivyo ni muhimu wakajifunza kikamilifu matumizi ya teknolojia hiyo,” alisema Dk Maleko

Mkutano wa 58 wa magavana wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Dunia umezishirikisha nchi 54 za Bara la Afrika.

Chanzo: www.habarileo.co.tz