Mamlaka nchini Msumbiji zimesema karibu wanamgambo 90 wa Kiislamu pamoja na mateka wao wamejisalimisha kwa serikali katika kipindi cha miezi miwili iliyopita huko Mocimboa da Praia katika jimbo la Cabo Delgado.
Jimbo hilo limekabiliana na uasi wa kikatili wa wanajihadi ambao umesababisha mzozo mkubwa wa kibinadamu kaskazini mwa Msumbiji.
Rais Filipe Nyusi mwezi Septemba alitangaza msamaha kwa wanajihadi wote waliojisalimisha wakati wa ziara yake katika jimbo hilo.
Tangu mwaka 2017, wanamgambo wamefanya ukatili mkubwa ikiwemo utekaji nyara, kukata watu vichwa, na kuchomwa kwa nyumba katika jimbo hilo na kuwalazimisha mamia kwa maelfu kukimbilia usalama wao.