Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Magaidi 12 Al-Shabaab wauawa Somalia

Jeshi Alshabab Somalia Jeshi laua magaidi 12 wa Al-Shaabab

Tue, 14 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jeshi la taifa la Somalia siku ya Jumatatu lilisema kuwa lilifanya operesheni dhidi ya kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye mafungamano na al-Qaeda katika eneo la kati la Hiran, na kuua takriban magaidi 12 wa kundi hilo la magaidi wakufurishaji.

Operesheni hiyo iliyoendeshwa na askari wa kikosi maalumu jeshini ilifanyika karibu na mji wa Mataban katika eneo la kati la Hiran mwishoni mwa Jumapili.

"Magaidi 12 wa Al-Shabab waliuawa katika operesheni iliyoendeshwa na Jeshi la taifa la Somalia karibu na kijiji cha Qabdho kilichoko wilayani Mataban mkoa wa Hiran katika muda wa saa 24 zilizopita," Shirika la Habari la Taifa la Somalia liliripoti.

Brigedia Jenerali Odowa Yusuf Rageh, kamanda wa jeshi la taifa la Somalia aliyezungumza na redio ya jeshi, amethibitisha operesheni hiyo, akisema lengo kuu ni kuharibu maficho ya magaidi na kuzuia njama zao.

Amesema kuwa wakati wa operesheni hiyo, jeshi liliharibu kambi ya al-Shabaab huko Qabdho nje kidogo ya Mataban, ambapo magaidi wa al-Shabaab walikuwa wakipora pesa kutoka kwa watu wa eneo hilo.

Mataban, ni mji unaopatikana kilomita 405 (maili 251) kutoka mji mkuu Mogadishu.

Hayo yanajiri siku kadhaa baada ya Rais mpya wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud kuahidi kukabiliana na ugaidi katika nchi hiyo iliyokumbwa na mzozo, huku pia akiiomba jamii ya kimataifa iisaidie nchi hiyo dhidi ya tishio la baa la njaa.

Rais Mohamud amesema hayo wakati wa hafla ya kuapishwa kwake iliyofanyika Alkhamisi na kuahidi kuibadilisha Somalia kuwa "nchi ya amani" na kurekebisha uharibifu uliosababishwa na migogoro ya kisiasa ya miezi kadhaa.

Jeshi la Somalia linashirikiana na Askari wa Kikosi cha Mpito cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika (ATMIS) katika kukabiliana na magaidi hao wa al-Shabab. Kuna askari wapatao 20,000 kutoka Uganda, Ethiopia, Burundi na Kenya wanaohudumu katika kikosi hicho

Chanzo: www.tanzaniaweb.live