Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mafuriko yaua zaidi ya watu 600 Nigeria

Mafuriko Nigeria Mafuriko yaua zaidi ya watu 600 Nigeria

Mon, 17 Oct 2022 Chanzo: BBC

Mafuriko ya hivi majuzi nchini Nigeria yamekuwa "janga" kubwa, na majimbo mengi hayakuwa tayari kuyakabili licha ya onyo, waziri wa usimamizi wa majanga amesema.

Zaidi ya watu 600 wamefariki katika mafuriko mabaya zaidi kuwahi kutokea katika taifa hilo la Afrika Magharibi katika muongo mmoja uliopita.

Watu wapatao milioni 1.3 wamekimbia makazi yao, na zaidi ya nyumba 200,000 zimeharibiwa. Mafuriko yanatarajiwa kuendelea hadi mwisho wa Novemba. Nigeria imezoea mafuriko ya msimu, lakini mwaka huu imekuwa mbaya zaidi kuliko kawaida.

Serikali imesema mvua kubwa isiyo ya kawaida na mabadiliko ya hali ya hewa ndio ya kulaumiwa. Wataalamu pia wanasema mipango duni na miundombinu imezidisha uharibifu huo.

Mitumbwi na majirani wanaojali walikabiliana na mafuriko ya Nigeria Tangu mafuriko yaanze mwanzoni mwa msimu wa joto, maeneo makubwa ya mashamba yameharibiwa. Kuna wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa magonjwa, na usambazaji wa chakula na mafuta pia umetatizwa.

Katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumapili, waziri wa masuala ya kibinadamu na usimamizi wa majanga wa Nigeria, Sadiya Umar Farouk, alitoa wito kwa mamlaka za mitaa kuwahamisha watu wanaoishi katika maeneo hatarishi zaidi.

Mamlaka tayari zinatoa chakula na msaada mwingine kwa wale walioathirika, alisema. Aliongeza kuwa licha ya ''juhudi za pamoja'' na maonyo ya mapema, serikali nyingi za majimbo "hazikujiandaa" kwa mafuriko. Maafa hayo yameathiri majimbo 27 kati ya 36 ya Nigeria.

Sehemu ya tatizo ni kwamba watu hurudi makwao kwenye nyanda za mafuriko kila mwaka baada ya maji kupungua. Wengi hawana njia za kuhama. Uchumi wa Nigeria umedorora katika mwaka uliopita, huku mfumuko wa bei ukiwa juu sana na jamii nyingi zikijitahidi kustahimili.

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo lilisema mwezi uliopita kuwa Nigeria ni miongoni mwa nchi sita zinazokabiliwa na hatari kubwa ya janga la njaa.

Shirika la hali ya hewa la Nigeria limeonya kuwa mafuriko yanaweza kuendelea hadi mwisho wa Novemba katika baadhi ya majimbo ya kusini mwa nchi hiyo, yakiwemo Anambra, Delta, Rivers, Cross River na Bayelsa.

Chanzo: BBC