Idadi ya watu walioaga dunia kwa janga la mafuriko nchini Somalia inazidi kuongezeka huku athari mbaya za mafuriko hayo zikizidi kudhihirika katika nchi hiyo inakabiliwa pia na baa la njaa.
Duru za kieneo zinasema, karibu watu 100 wamefariki dunia nchini humo kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha katika baadhi ya maeneo ya nchi hyo.
Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limetangaza pia kuwa, mafuriko yaliyoikumba Somalia katika siku za hivi karibuni yamesababisha kwa akali watu nusu milioni kubaki bila makazi kutokana na nyumba zao kubomolewa au kujaa maji kiasi cha kutokalika.
Mafuriko hayo ni mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini Somalia katika karne moja iliyopita.
Mafuriko makubwa yaliyoikumba Somalia mbali na kusababisha vifo na uharibifu mkubwa yamesomba makaburi katikati mwa jiji la Galkayo na kuacha miili ikielea mitaani.
Hivi majuzi kuonekana kwa miili iliyofukuliwa na mafuriko kuliwatisha wakazi wa mji huo hasa wanaoishi katika maeneo yaliyo karibu na makaburi.
Baadhi ya miili hiyo ilitambulika, na kuwatia kiwewe zaidi watu na maji yanapopungua mifupa iliyofukuliwa pia huonekana.
Umoja wa Mataifa unaonya kuwa zaidi ya watu milioni 1.6 wanaweza kuathiriwa na mafuriko makubwa ambayo yanakuja baada ya nchi hiyo kukumbwa na ukame wa miaka mingi.
Tangu mwanzoni mwa mwezi huu, mvua kali zimeikumba Somalia na majirani zake Kenya na Ethiopia, na kusababisha maporomoko ya ardhi na kuzamisha vijiji na mashamba.
Mafuriko hayo yanakuja baada ya Somalia na baadhi ya maeneo ya Ethiopia na Kenya kukumbwa na ukame mkubwa kuwahi kushuhudiwa katika eneo hilo katika miongo minne iliyopita.