Takribani watu 30,000 wamehamishwa kutoka katika mji wa Derna ambao umeathirika vibaya zaidi na mafuriko makubwa yaliyoikumba Libya.
Maafisa wa afya wamesema kuwa idadi ya vifo katika mji huo imeongezeka na kufikia 5,300 na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka. Baadhi ya miili imeanza kuzikwa kwenye makaburi ya halaiki.
Mapema jana Uingereza ilitangaza kupeleka misaada nchini Libya yenye thamani ya takribani pauni milioni 1 ili kusaidia mahitaji ya walioathirika na maafa hayo.
Kupitia mtandao wa X Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak amesema ”inashtua kuona kiwango cha vifo na uharibifu uliosababishwa na mafuriko nchini Libya. Uingereza inajipanga kutoa msaada wa haraka”.
Maafisa nchini Libya wameomba msaada kutoka Mataifa ya nje na kueleza kuwa nchi yao haina uzoefu wa kushughulika na maafa ya kiwango hiki.