Madereva wa masafa marefu wamelaumiwa kwa kuwa miongoni mwa watu ambao wanasambaza kunguni na mende.
Hawasafishi magari, labda yanyeshewe hivyo basi kuchochea mazingira mazuri kwa wadudu hao kuzaana.
“Mara tu baada ya kupika wanarundika vyombo vya kupikia ndani ya gari na huviacha kukaa hapo kwa siku kadhaa kabla ya kuoshwa,” anasema Dennis Wambua. Isitoshe, baadhi hutumia pesa za kuosha magari (car wash) kununua miraa, maarufu kama jaba kwa lugha ya mtaa.
Wambua ambaye ni dereva kutoka Bandari ya Mombasa hadi Busia, kwenye mahojiano na Taifa Leo Dijitali alidai hali ngumu ya maisha ndiyo inasukuma baadhi ya madereva kuishi kama ndege ndani ya kiota.
“Pesa za matumizi ni kidogo mahitaji yakiwa mengi mno,” akasema. Aidha, Taifa Leo Dijitali ilisaka maoni kutoka kwa wanotoa huduma za kusafisha magari katika kituo cha kibiashra cha Sultan Hamud.
Baadhi yao wanaungama kwamba biashara ya kusafisha magari ya uchukuzi wa masafa marefu si nzuri, labda mara mojamoja.
“Wateja wetu wengi ni wamiliki wa magari madogo ya uchukuzi kwa ajili ya familia hasa wikendi,” anasema Ernest Mwangi.
Kulingan na Mwangi, bei ya kusafisha matrela ya masafa marefu huwa ni ghali ikilinganishwa na ile ya magari madogo aghalabu madereva wakitozwa kati ya Sh1, 000 hadi Sh1, 200.
Mwangi anasema siku za baadaye, wasafishaji malori huenda wakapandisha bei kwa sababu ya gharama ya juu ya mafuta, ikizingatiwa kuwa wao hutumia mtambo wa umeme kuendesha jenereta ya kuosha magari.
Kupitia mtandaoni, DJ Marcus anasema ukiingia ndani utakumbana na harufu kali. Isitoshe, anakiri kwamba kunguni na mende hutembea waziwazi kutoka sehemu moja ya gari hadi nyingine.