KITISHO cha virusi vya corona na mazingira mabovu ya kufanyia kazi, ni miongoni mwa mambo yanayofanya shughuli za utoaji huduma za afya kuwa ngumu na kuzua malalamiko kutoka kwa madaktari na wauguzi.
Kutokana na hali hiyo, madaktari nchini humo wametangaza kuanza mgomo baada ya wiki mbili zijazo iwapo hawataongezewa mishahara na vitendea kazi vyao kutoimarishwa hasa katika kipindi hiki ambacho nchi hiyo inakabiliwa na janga la virusi vya corona.
Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari Kenya, Chibanzi Mwachonda, akizungumza na waandishi wa habari alisema wamechoka na ahadi za serikali ambazo hazitekelezwi licha ya mkataba wa kuongezewa mshahara kutiwa saini mwaka 2017.
Tishio hilo la madaktari kugoma, limekuja wakati huu nchi hiyo ikiwa katikati ya mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.
Hivi karibuni, wauguzi wanaofanya kazi katika wodi iliyotengwa kwa ajili ya watu walioambukizwa virusi vya corona walifanya mgomo baridi, wakilalamikia ukosefu wa vifaa vya kujikinga na kutopatiwa mafunzo ya kujilinda na virusi vya corona.