Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madaktari waomba chanjo ya Mpox ifike DR Congo

Madaktari Waomba Chanjo Ya Mpox Ifike DR Congo .png Madaktari waomba chanjo ya Mpox ifike DR Congo

Wed, 11 Sep 2024 Chanzo: Bbc

Wahudumu wa afya wanaopambana kukabiliana na ugonjwa wa mpox mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wameiambia BBC kwamba wanatamani chanjo kufika eneo hilo ili waweze kuzuia kasi ya maambukizi mapya.

Katika kituo cha matibabu katika jimbo la Kivu Kusini ambacho BBC ilitembelea kwenye kitovu cha mlipuko huo, wanasema wagonjwa zaidi wanafika kila siku - hasa watoto wachanga - na kuna uhaba wa vifaa muhimu.

Mpox - ambayo zamani ilijulikana kama monkeypox - ni ugonjwa unaoambukiza sana na umeua takriban watu 635 nchini DR Congo mwaka huu.

Ingawa chanjo 200,000, zilizotolewa na Tume ya Ulaya, zilisafirishwa hadi mji mkuu, Kinshasa, wiki iliyopita, bado hazijasafirishwa katika maeneo ya nchi hii kubwa - na inaweza kuchukua wiki kadhaa kabla ya kufika Kivu Kusini.

"Tumejua kupitia mitandao ya kijamii kwamba chanjo hiyo tayari inapatikana," Emmanuel Fikiri, muuguzi anayefanya kazi katika kliniki hiyo ambayo imegeuzwa kuwa kituo maalum cha kukabiliana na virusi hivyo, aliiambia BBC.

Alisema hii ni mara yake ya kwanza kuwatibu wagonjwa wa mpox na kila siku aliogopa kupata maambukizi hayo na kuyasambaza hadi kwa watoto wake wa miaka saba, mitano na mmoja.

“Uliona jinsi nilivyowagusa wagonjwa kwa sababu hiyo ndiyo kazi yangu kama muuguzi. Kwa hiyo, tunaiomba serikali itusaidie kwa kutupa kwanza chanjo hizo.”

Sababu itachukua muda kusafirisha chanjo hizo ni kwamba zinahitaji kuhifadhiwa kwenye halijoto halisi – ikiwa kiwango cha joto cha baridi - ili kudumisha nguvu yake, pamoja na kutumwa katika maeneo ya vijijini ya Kivu Kusini, kama vile Kamituga, Kavumu na Lwiro, ambapo mlipuko huo umeenea.

Chanzo: Bbc