Kundi la madaktari nchini Uganda lilizua tafrani mwishoni mwa juma baada ya kupiga magoti mbele ya Rais wa muda mrefu Yoweri Museveni na kumtaka agombee muhula wa saba.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 78 amekuwa madarakani tangu 1986. Uchaguzi mkuu ujao WA Uganda unatarajiwa kufanyika mwaka wa 2026.
Madaktari wanaowakilisha Chama cha Madaktari Uganda (UMA) walikuwa wamehudhuria kongamano la uzalendo katika mji mkuu, Kampala, walipoongozwa na kiongozi wao kupiga magoti mbele ya rais, kulingana na picha za vyombo vya habari za tukio hilo.
Katika hotuba yake, mkuu wa UMA Dkt Samuel Odongo Oledo alimsifu rais kwa kubadilisha mfumo wa afya nchini na kuboresha ustawi wa wafanyakazi wa matibabu, tovuti ya habari ya Nile Post inaripoti.
Aliendelea kumwomba Rais Museveni kuwania tena 2026 kama mgombeaji urais, kituo cha televisheni cha NTV kinaripoti.
Kitendo hicho kilizua mijadala kwenye mitandao ya kijamii huku wengi wakilishutumu kundi hilo kwa kuwatii wanasiasa.
Lakini katika ukurasa wa Twitter wa UMA ilijitenga na ishara hiyo, ikisema "haikuwakilisha njia za uendeshaji wa chama".
Ilisema: "Chama cha Madaktari wa Uganda siku zote kimekuwa kikishirikiana na rais kwa njia rasmi, za kitaalamu ikiwa ni pamoja na kumthamini kupitia tuzo zetu za kila mwaka."