Mamlaka Huru ya Kuangalia Utendaji kazi wa Polisi – IPOA, kupitia Mwenyekiti wake, Anne Makori imesema imeanza uchunguzi kuhusu kisa cha Polisi kuwapiga risasi na kuwaua watu sita, katika Kaunti ya Migori nchini Kenya.
Inadaiwa watu hao sita walikuwa miongoni mwa watu waliovamia kituo cha Polisi cha Isebania wakiwa wamejihami kwa mapanga na mawe wakiwa na hasira kali kwenye msafara uliokuwa umetoa mwili wa mkazi mmoja kutoka kwenye hifadhi moja ya maiti.
Taarifa zinasema, watu hao walipofika kituoni, walivamia wakitaka majibu ni kwa nini kumekuwa na visa vya utovu wa usalama katika sehemu hizo na kisha kuanza kuyavunja madirisha na milango ya kituo hicho huku wakiwa na lengo la kuiba bunduki na kuwafungulia watuhumiwa waliokuwa selo.
Aidha, mara baada ya kuona wamezidiwa nguvu na ghala la silaha limevamiwa, Polisi hao walifyatua risasi kujaribu kuwatawanya lakini wakadai kwa bahati mbaya risasi hizo zilileta maafa.
Katika taarifa yake, IPOA imesema ilifahamu kisa cha ufyatuaji risasi katika kituo cha polisi cha Isebania katika Kaunti Ndogo ya Kuria Magharibi, ambapo watu sita waliripotiwa kuaga dunia na wengine wakajeruhiwa vibaya.