Kiongozi wa madhehebu ya Shakahola Paul Mackenzie na washtakiwa wenzake 38 wamekana mashtaka ya ukatili wa watoto na kukiuka haki za watoto.
Mackenzie na watuhumiwa wenzake, wanaokabiliwa na makosa 16, likiwemo la kutesa watoto, wanadaiwa kutenda makosa hayo kwa tarehe tofauti kati ya 2020 na 2023 katika Msitu wa Shakahola.
Mnamo Alhamisi, Mackenzie, ambaye aliongoza Kanisa la Good News International, na washtakiwa wenzake walikanusha makosa yote waliyoelekezwa walipofika mbele ya Mahakama ya Watoto ya Tononoka.
Hakimu Mkuu Nelly Chepchirchir aliongoza kesi hiyo.
Katika shtaka la utesaji wa watoto, Mackenzie na washtakiwa wenzake walishtakiwa kwa kuwapiga makofi na kuwachapa watoto wa kati ya miaka 8 na 14, na hivyo kuwadhuru mwili kwa tarehe tofauti.
Shtaka hilo kwa kiasi lilisema, “Paul Nthenge Mackenzie, almaarufu Mtumishi almaarufu Nabii almaarufu Papaa, tarehe zisizojulikana mwaka wa 2019 katika Kaunti ya Kilifi, kwa makusudi alimtoa mtoto wa miaka kumi na tatu (13) kutoka Shule ya Msingi ya Inavi na akashindwa kuhakikisha kwamba mtoto huyo anahudhuria shule mara kwa mara kama mwanafunzi."
Kesi inayomkabili Mackenzie na washtakiwa wenzake itatajwa Februari 15, maombi ya dhamana yatakaposikilizwa.
Mnamo Januari 23, Mackenzie, pamoja na mkewe na washtakiwa wengine 93, walishtakiwa kwa kuua bila kukusudia katika mahakama ya Mombasa.
Wote walikana mashtaka 238. Wiki iliyopita, Mackenzie na washirika wake walishtakiwa kwa makosa yanayohusiana na ugaidi mbele ya Mahakama ya Shanzu, ambayo wote walikana.