Mhubiri mwenye utata Paul Mackenzie na washtakiwa wenzake katika kesi ya mauaji ya Shakahola wamefika katika Mahakama Kuu ya Mombasa kufahamishwa kuhusu hatma ya ombi lao la dhamana.
Baadhi ya wafuasi wa Mackenzie Good News International Ministries hata hivyo walionekana dhaifu kutokana na mgomo wa chakula.
Baadhi walionekana kushindwa kusimama kizimbani na ilidaiwa kuwa walikuwa kwenye mgomo wa kula na walikuwa hawajala kwa siku tatu zilizopita.
Jaji wa Mahakama Kuu Alex Ithuku aliwaagiza kukaa katika eneo la mahakama na kuwakilishwa katika kesi hiyo na wakili wao.
Wakati wa kufikishwa mahakamani wiki iliyopita, Mackenzie na washtakiwa wenzake 38 walishtakiwa kwa makosa 17 ikiw ani pamoja na kuwatesa watoto, kuwashambulia, kuwafanyia ukatili na kukiuka haki ya mtoto ya kupata elimu.
Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma ilisema inataka mahakama iwanyime washukiwa dhamana kwa madai kwamba kuna hatari iwapo wangeachiliwa.