Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Machi: Mwezi wa utekaji nyara watu wengi nchini Nigeria

Wakimbizi Wa Ndani Watekwa Nyara Nchini Nigeria Machi: Mwezi wa utekaji nyara watu wengi nchini Nigeria

Thu, 21 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jeshi la Nigeria limetangaza kuwa lilifanikiwa "kuepusha jaribio la utekaji nyara" na kuwazuia waathiriwa 16 kutekwa kutoka kwa jamii katika eneo lenye matatizo la Kajuru katika Jimbo la Kaduna, kaskazini-magharibi mwa nchi, Jumapili usiku.

Lakini usiku huo huo, magaidi walishambulia jamii nyingine ya Kajuru na kuwateka nyara makumi ya watu.

Katika muda wa wiki mbili zilizopita, kaskazini mwa Nigeria kumeshuhudia mashambulizi sita yakisababisha utekaji nyara wa watu wengi.

Tukio hili la hivi punde linaangazia jinsi magenge ya wahalifu wenye jeuri, wanaoshukiwa kuwa na uhusiano na kundi la Ansaru lenye uhusiano na al-Qaeda, wameongeza shughuli zao katika eneo hili.

Imekuwa changamoto kwa wiki mbili kwa serikali ya Nigeria, ambayo imelazimika kutumia rasilimali zaidi za usalama kujaribu kuokoa mamia ya waathiriwa waliotekwa nyara.

Hadi sasa, hakuna mwathirika hata mmoja aliyepatikana.

Kuongezeka kwa uvunjaji wa sheria kunaonyesha jinsi magenge ya wahalifu wenye silaha yanavyodhibiti vikosi vya usalama vya Nigeria, ambavyo vimesalia nyuma.

Wengi wameshutumu mamlaka kwa kutochukua hatua haraka vya kutosha na hivyo kusababisha matukio ya vurugu zaidi.

''Serikali haiko makini kuhusu kulinda maisha na mali. Viongozi hawaweki hilo kwenye orodha ya vipaumbele vyao. Ikiwa walikuwa makini, tungeona mabadiliko. Tungeona kuboreshwa kwa usalama,'' Isa Sanusi, Mkurugenzi wa shirika la Amnesty International wa Nigeria, aliambia BBC News.

Utekaji nyara wa kwanza mwezi huu ulifanyika mnamo Machi 6 katika Jimbo la Borno kaskazini-mashariki. Watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo walishambulia mji wa mbali na kuwateka nyara takriban watu 200, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, kutoka katika kambi ya wakimbizi wa ndani walipokuwa wakitafuta kuni.

Licha ya kuanzisha "operesheni ya utafutaji na uokoaji", jeshi lilishindwa kuwarudisha waliotekwa nyara.

Siku iliyofuata mnamo Machi 7, karibu wanafunzi 300 na walimu walitekwa na watu wenye silaha kutoka shule ya Kaduna. Serikali ya jimbo hilo baadaye ilitangaza kuwa wanafunzi 28 walitoroka watekaji wao.

Katika taarifa yake, Mwakilishi wa UNICEF nchini Nigeria, Cristian Munduatehe alilaani ''matukio ya kutisha ya matukio kama haya kote nchini'' akisema ''inaashiria mgogoro ambao unahitaji hatua za haraka na zilizoazimiwa kutoka ngazi zote za serikali na jamii.''

Mnamo Machi 9, watu wenye silaha waliwateka nyara takriban wanafunzi 15 kutoka shule nyingine katika jimbo la Sokoto kaskazini magharibi mwa Nigeria katika uvamizi uliofanyika nyakati za alfajiri.

Siku mbili baadaye, watu wanaoshukiwa kuwa majambazi walishambulia tena eneo la serikali ya mtaa wa Kajuru katika Jimbo la Kaduna, na kuwateka nyara watu 61.

Mashambulizi ya hivi punde pia yalitokea Kajuru, huku zaidi ya watu 100, wakiwemo wanawake na watoto, wakichukuliwa na magaidi.

Hakikisho la Rais Bola Tinubu kuwapa uwezo wanajeshi kukabiliana na ukosefu wa usalama umewekwa chini ya uangalizi wa karibu kutokana na utekaji nyara wa watu wengi. Licha ya maombi ya mara kwa mara ya BBC, maafisa wameshindwa kutoa maoni yao kuhusu mipango yao ya kukabiliana na hali hii inayoongezeka ya utekaji nyara.

Haijabainika kwa nini kumekuwa na ongezeko la utekaji nyara hivi karibuni, lakini kumekuwa na ripoti huko nyuma ambapo wanawake waliotekwa walilazimishwa kuwapikia watekaji wao.

Watu wenye silaha wameomba fidia ili kuwaachilia wanafunzi waliotekwa nyara mapema mwezi huu, lakini mamlaka inasisitiza hakuna pesa zitakazolipwa. Utekaji nyara kwa ajili ya fidia ni jambo la kawaida nchini Nigeria, lakini kulipa ni kinyume cha sheria.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live