Wachuuzi wa ngono katika kaunti ya Tana River wametangaza kupandisha bei ya huduma zaokatika kile ambacho walikitaja kuwa ni sababu za kupanda kwa gharama ya maisha nchini, jarida la Taifa Leo limeripoti.
Kwa mujibu wa tangazo hilo amablo lilionekana na jarida hilo, ina maana kuwa wanaosaka huduma za ngono hawatakuwa na budi ila kufukua mfuko zaidi kugharamia starehe.
Mkuu wa kundi la vidosho hao katika kaunti hiyo kwa njia ya simu aliambia jarida hilo kuwa kuanzia mwezi Agosti bei ya huduma za kushiriki mapenzi zitaongezeka kwa asilimia kumi, kwani pesa walizokuwa wakitoza haziwezi kamwe kukimu mahitaji yao kama hapo awali.
“Bei ya mipira (kondomu) imepanda, sawa na mahitaji mengine ya kimsingi kama vile chakula na maji. Wamiliki wa madanguro pia wanapandisha bei ya vyumba, sasa nasi inatubidi kupandisha,” aliambia Taifa Leo Dijitali.
Kiongozi huyo wa kundi la wachuuzi hao anaelezea kuwa hali inazidi kuwa ngumu, na hivyo kuwataka wateja kuelewa na kukubali hali halisi.
Aliambia jarida hilo kwamba, ili kuhakikisha kuwa biashara hiyo inafana na kila mtu anaridhika, bei ya ngono haitapungua Sh500.
“Sote tunasaka riziki na ikiwa unataka nikufurahishe, huna jingine ila nawe pia unifurahishe. Maelewano ya chini sana yasipungue Sh500, na tutawachunguza wenzetu kuhakikisha tunazungumza lugha moja,” alinukuliwa na jarida hilo.
Wachuuzi hao wa ngono wametoa notisi ya kuongeza bei za huduma zao ikiwa ni wiki chache tu baada ya mchekeshaji Jaymo Ule Msee kutoa ombi kwa serikali kuweka ushuru kwa huduma hizo, akisema kuwa ni vyema kutozwa ushuru kama kweli wanataka serikali itambue na kulinda riziki zao.
Nchini, gharama ya maisha inazidi kutekenya kila upande, huku mfumko wa bidhaa muhimu ukizidi kuwa shubiri kwa wengi.