Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mabadiliko Itifaki SADC yalete tija kwa wanachama

5c921725614200e46ec05d963ac21d98.jpeg Mabadiliko Itifaki SADC yalete tija kwa wanachama

Wed, 5 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MAOFISA Waandamizi wa Sekta ya Sheria wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) walikutana juzi kwa njia ya mtandao kujadili mambo mbalimbali ikiwemo maboresho ya Itifaki zilizoonekana kuwa na upungufu katika utekelezaji wake.

Katika mkutano huo uliowahusisha makatibu wakuu na manaibu wanasheria wakuu wa serikali zote 16 za SADC, ulibainisha pia kuwa kumekuwa na kasi ndogo ya nchi za jumuiya hiyo katika kuridhia Itifaki mbalimbali, hivyo hatua imechukuliwa ya kupitia upya Itifaki tatu.

Itifaki hizo ni pamoja na ya silaha ili kuiongezea nguvu katika kudhibiti silaha haramu katika ukanda huo. Nyingine ni inayohusu masuala ya Kazi na Ajira ambayo imekuwa ngumu kutekelezeka na kupendekezwa ifutwe na kuundwa mpya na ya tatu ni Itifaki ya Takwimu ambayo imerejeshwa katika ngazi ya kisekta iangaliwe tena.

Hii ni kudhihirisha kuwa, utekelezaji wa mapendekezo zaidi ya 30 yaliyotolewa na Wakuu wa Nchi za SADC katika Mkutano wao Mkuu wa Agosti mwaka jana (2019) uliofanyika jijini Dar es Salaam ambao pamoja na mambo mengine uliazimia kudhibiti ugaidi na silaha haramu, umeanza.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome ndiye aliyeeleza hayo kwa waandishi wa habari, alipozungumza nao juzi jijini Dar es Salaam wakati mkutano huo ukiendelea kwa njia ya mtandao.

Kwa mujibu wa Profesa Mchome, ambaye ni Mwenyekiti wa Maofisa Waandamizi wa SADC sekta ya Sheria, kusuasua kwa nchi wanachama katika kuridhia itifaki mbalimbali kunatokana na mapungufu ya itifaki hizo na mlolongo wa kuridhiwa uliopo katika kila nchi.

Kwa mfano, kwa Tanzania, Itifaki zinaporidhiwa na Jumuiya, nyingi lazima zipelekwe kwanza bungeni zipate ridhaa ya Bunge ndio zitumike. Hali hii ipo kwa kila nchi huku wengine wakipaswa kuzipeleka katika Baraza la Mawaziri kwanza.

Kwa upande wa Itifaki ya Silaha, Profesa Mchome anakiri kwamba ina upungufu hivyo wanataka iongezewe nguvu ili kudhibiti zaidi silaha ndogo ndogo haramu zinazoingia katika nchi za SADC kinyemela.

Kuhusu Itifaki ya masuala ya Kazi, hii imekuwa ngumu kutekelezeka, hivyo Maofisa Waandamizi wamependekeza kwa mawaziri wa SADC wa Sheria itifaki hiyo ifutwe na kuanza kazi ya kuandaa nyingine.

Itifaki ya tatu iliyojadiliwa juzi ni ya Takwimu, hii ina mapendekezo mapya yanayopaswa kuingizwa hivyo wameirejesha kwenye ngazi ya sekta ili iangaliwe upya na wadau kutoka nchi zote wanachama wapate nafasi ya kutoa mapendekezo yao.

Hatua hizi za michakato ya kuboresha itifaki hizi inatia moyo na kwa hakika ina nia njema ndani yake. Kikubwa ambacho nakitamani katika michakato hii ni kuhakikisha inaleta tija kwa kila nchi mwanachama, hali itakayoondoa kigugumizi na milolongo ya kuziridhia Itifaki hizo kwa kila nchi.

Kazi ya kuzipitia na kuziboresha si ndogo, inahitaji ushiriki mkubwa wa nchi wanachama ili kupata itifaki zinazogusa wote na kwa manufaa ya wote, ikiwa lengo kweli ni kuongeza nguvu katika udhibiti wa silaha, kupanua wigo wa upatikanaji wa ajira na masuala mengine yanayohusu mustakabali wa jumuiya hiyo.

Chanzo: habarileo.co.tz