Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maandamano ya Gen Z yanavyozidi 'kuvuna' kutoka serikali ya rais Ruto

Magenge Ya Haiti Yamtaka Waziri Mkuu Ajiuzulu Baada Ya Kuvamiwa Kwa Gereza Maandamano ya Gen Z yanavyozidi 'kuvuna' kutoka serikali ya rais Ruto

Tue, 16 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hatua ya hivi punde ya rais wa Kenya William Ruto kulivunja baraza lake la mawaziri imetajwa kuwa miongoni mwa mafanikio ambayo yameletwa na maandamano ya vijana wa Gen Z nchini Kenya . Maandamano yao yalikuwa mwanzo wa hatua ambazo zimeifikisha kenya hadi katika hatua hii ya hivi punde .

Mwanzoni walipuuzwa kama vijana wavivu ambao muda wao mwingi waliiutumia katika mitandao ya kijamii.

'Mara moja nitashiriki katika mashauriano ya kina katika sekta mbalimbali na miundo ya kisiasa, kwa lengo la kuunda serikali pana ambayo itanisaidia katika kuongeza kasi na kuharakisha yanayohitajika, ya haraka pamoja na utekelezaji wa mipango mikali ya kukabiliana na mzigo wa madeni, kuongeza rasilimali za ndani, kupanua nafasi za kazi, kuondoa uharibifu wa fedha na marudio yasiyo ya lazima ya msururu wa vyombo vya serikali na kuua joka la ufisadi hivyo kuifanya serikali kuwa isiyo na gharama kubwa , na yenye ufanisi' ,rais amesema katika hotuba yake kwa taifa.

Wakati walipoamua kutekeleza hatua yao ya kwenda barabarani ili kulalamikia mswada wa fedha uliokuwa ukipendekeza nyongeza ya ushuru kwa bidhaa mbalimbali,wengi waliwapuuza na hawakujua athari za walichokianzisha.

Lakini sasa ni wazi kwamba licha ya maandamano ya vijana wa Kenya wa kizazi cha Gen Z kuingiliwa na makundi ya uhalifu na magenge ya uporaji-kuna mazuri ambayo yametokea kwa sababu ya hatua ya vijana hao.

Serikali na uongozi wa nchi sasa unaonekana kuchukua kila hatua kwa uangalifu. Miongoni mwa mambo ambayo huenda yaliwashtua wengi,ni viongozi wa kisiasa kujitokeza na kukataa nyongeza ya mishahara iliyopendekezwa na Tume ya mishahara ya nchi hiyo SRC.

Je, Gen Z wamefaulu kuleta matumaini ya mageuzi na 'nidhamu' katika utawala wa Kenya?

Rais wa Kenya William Ruto ametaka kuangaliwa upya mara moja kwa mapendekezo ya nyongeza ya mishahara kwa maafisa wa serikali Hili huenda ndilo kubwa zaidi ambalo limetokana na shinikizo ya wananchi na hasa kutokana na maandamano ya hivi karibuni .

Ndio hatua muhimu inayoonekana kujibu lalama za wengi nchini humo ambazo zinahusu watu katika nyadhifa kuu serikalini kuwatwika mamilioni ya wananchi mzigo wa kugharamia mishahara yao ya juu na maisha ya kifahari.

Kando na rais William Ruto kulazimika kuufutilia mbali mswada wa fedha uliowasha maandamano hayo,hatua hii ya hivi punde inaingia katika orodha ya 'ushindi' wa waandamanaji.

Ingekuwa ajabu iwapo wabunge,maseneta na rais wangesalia kimya na kuendelea na mambo kama kawaida iwapo notisi hiyo ya SRC ya kuwaongeza maafisa wakuu serikalini mishahara ingetekelezwa .

Viongozi wengi kwa kauli moja waliikemea hatua hiyo ya SRC kutoa notisi ya nyongeza ya mishahara wakati huu hasa baada ya maandamano ya wanancha na wakikariri msimamo wa rais Ruto kwamba uchumi kwa wakati huu hauna nguvu kuweza kubeba mzigo wa nyongeza hiyo.

Kenya kwa sasa inatumia zaidi ya shilingi trilioni moja kuwalipa wafanyakazi wa umma, na kuna ongezeko la shilingi bilioni 29 la fedha zinazolipwa kama mishahara kwa watumishi wa umma licha ya tume ya mishahara kuzuia nyongeza ya hivi punde. . Mabadiliko katika baraza la mawaziri

Polisi wa Kenya wameshutumiwa kujibu maandamano hayo kikatili Iwapo kuna hatua ya wazi ambayo inasubiriwa na Wakenya wengi na hasa waliokwenda barabarani kuandamana ni iwapo rais atadhihirisha kwamba alisikia kilio chao kuhusu utendakazi wa baadhi ya mawaziri wake na baadhi ya maafisa wa ngazi za juu katika utawala wa muungano wa Kenya Kwanza .

Baraza jipya la mawaziri wenye uwezo wa kushughulia kero zao kitaalam ndio itakayokuwa zawadi bora kwa Wakenya . Rais tayari amechukua hatua ya kulivunja baraza hilo isipokuwa Kiongozi wa mawaziri Musalia Mudavadi na Naibu wa rais William Ruto.

Wengi wanasubiri kuona idadi ya mawaziri na sura ambazo rais Ruto atazileta serikalini na huenda akajipata pabaya zaidi iwapo atarejesha nyuso zile zile na kuziweka katika wizara tofauti.Mazungumzo kuhusu serikali 'pana' na ya 'umoja wa kitaifa' pia yanachukuliwa kwa uangalifu sana kwani huenda hilo likamaanisha idadi zaidi ya maafisa wa ngazi ya juu .

Mwisho wa siasa makanisani?

Iwapo kuna ushirikiano ambao unaonekana kuwaghadhabisha wengi nchini Kenya ,ni ule kati ya viongozi wa kisiasa na wa kidini .

Vijana waliokuwa wakiandamana wiki mbili zilizopita walikemea vikali ushirikiano huo ambapo kwa kawaida wanasiasa nchini Kenya wamekuwa na nafasi ya wazi ya kutumia kumbi za kidini na hasa makanisa kupiga siasa,kurushiana cheche za maneno na kila aina ya matamshi ambayo hayafai kutolewa kanisani.

Kupitia kauli yao ya #Occupychurches walianza kuwazuia wanasiasa dhidi ya kuwahutubia waumini makanisani.

Ujumbe wa vijana unaonekana ulichukuliwa kwa uzito na viongozi wengi wa makanisa ambao sasa wamewapa notisi wanasiasa kwamba hali haitakuwa kama ya kawaida .

Hili ni jambo ambalo litachukuliwa kama ushindi kwa waandamanaji wa Gen Z kwani ulikuwa mtindo wa kawaida kila Jumapili kuchanganya dozi ya injili na ile ya siasa .

Kwa muda mrefu hatua hiyo iliwakera wengi na sauti za pingamizi zimekuwa wazi katika maandamano hayo .

Viongozi wa kidini pia wameshtumiwa kwa kusalia kimya wakati serikali ilipokuwa ikipendekeza sheria kali za ushuru ambazo zilionekana kuwaacha wengi katika hali mbaya kiuchumi katika mazingira ambayo tayari gharama ya maisha imewalemea wengi .

Iwapo viongozi wa kidini watataka kusalia na hadhi ya kuheshimika katika jamii,watalazimika kuchukua hatua za wazi kujitenganisha na ushirikiano wao na wanasiasa na kupaza sauti zao kupinga kinachotafsiriwa mara nyingi kama uovu wa watawala .

Michango ya Harambee Iwapo kuna kichocheo cha wazi kwa maandamano ya vijana ,ni hatua ya wanasiasa na watumishi wa serikali walio karibu na viongozi wakuu wa nchi kuonekana hadharani wakibeba na kutoa vitita vya pesa katika michango -mara nyingi katika makanisa .

Maonesho hayo ya utajiri yameashiria kutojali kwa upande wa maafisa wa serikali wanaohusika na michango hiyo.

Katika nchi ambayo wengi wana matatizo ya kichumi,mabunda ya noti machoni mwa watu ambao wanatatizika kupata hata mlo mmoja kwa siku ni chanzo cha hamaki ambayo imetokota kwa muda .

Mlipuko wa hamaki hizo ulionekana katika maandamano ya vijana wa Gen Z.

Rais William Ruto aliahidi kwamba atachukua hatua kuhusu hilo wakati alipoashiria kwamba labda wakati umewadia kwa harambee kupigwa marufuku hasa kwa maafisa wa umma .

Michango kama hiyo inashukiwa kuchochea ufisadi na inahofiwa huenda fedha za umma ndizo hutolewa katika hafla hizo.

Baadhi ya viongozi pia hawajatuliza mambo kwa kupiga picha wakiwa katika magari ya kifahari, ziara za nje ya nchi na wakistarehe katika maeneo mbalimbali ya burudani .

Iwapo maandamano ya vijana yataleta kikomo kwa 'show' hizi kubwa za ni yupi aliye na hela nyingi ,gari kubwa au jumba bora la kifahari ,basi yatakuwa yamepata ufanisi wa kuleta aina fulani ya nidhamu.

Uwajibikaji wa kisiasa

,Linda Indakwa anatumia sanaa yake kuonyesha athari za maandamano katika mji mkuu Iwapo kuna ushindi mkubwa ambao utaletwa na hatua ya vijana kwenda barabarani ,basi kuleta uwajibikaji kwa viongozi waliochaguliwa ndio utakaokuwa ushindi muhimu sana .

Athari za mwamko huu mpya zimeanza kuonekana.

Pingamizi ya wananchi dhidi ya mswada wa fedha ilikuwa wazi.

Wananchi walituma jumbe kwa wabunge wao,walifoka mitandaoni na kupiga kila aina ya kelele kusikika ,lakini viongozi wa kisiasa walifumbia macho malalamishi hayo na kupitisha mswada huo .

Wabunge wengi waliopiga kura ya 'Ndiyo' sasa watakuwa na kazi ya kukutana na wapiga kura.

Baadhi yao wameanza kuomba msamaha kwa wapiga kura katika maeneo bunge yao .

Iwapo watasamehewa ama adhabu ya wapiga kura ipo njiani ,ni jambo litakalosuburiwa hadi uchaguzi wa mwaka wa 2027.

Tayari chama cha upinzani cha ODM kimesema kimeanzisha mchakato wa kuwarejesha nyumbani wabunge wake sita ambao walipiga kura ya kuunga mkono mswada huo wa fedha .

Makali ya ufanisi wa maandamano kuhusu kuwaajibisha viongozi wa kisiasa kwa kweli yatakuwa wazi wakati wa uchaguzi.

Iwapo kutakuwa na athari ya kampeni ya kuwataka viongozi kuwatumikia ifaavyo wananchi ,majibu yatakuwa wazi kupitia kura kwa sababu kwa muda mrefu wanasiasa wamekuwa wakitegemea sana usahaulivu wa wapiga kura .

Wakati huu ni wazi kwamba wanakabiliana na kizazi kisichosahau na chenye ushahidi unaowachwa kote mitandaoni kuhusu 'madhila' wanayotendewa na waakilishi wao.

Swali litakuwa iwapo 'ulimama na sisi' wakati wa matatizo yetu au ulikwenda kuyashughulikia maslahi yako binafsi.

Kubana matumizi ya fedha za umma Daalili nzuri ya uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma ilionekana pale rais William Ruto aliposisitiza kwamba sasa kuna haja ya dharura ya Kenya kubana matumzi ya fedha za umma .

Kwanza ameashiria kwamba huenda afisi zisizo za kikatiba kama ile ya Mke wa rais na mke wa naibu wa rais zikaondolewa na mgao wa bajeti kwa afisi hizo kuelekezwa kwa matumizi mengine .

Hatua hiyo haingechukuliwa endapo vijana wa kizazi Gen Z hawangeandamana na kuzua maswali muhimu sana kuhusu matumizi ya fedha zinazolipwa kupitia kodi na wananchi .

Ingawa rais Ruto ameelezea kwa kina athari za kukataliwa kwa mswada wa fedha ikiwemo serikali kupunguza migao kwa sekta muhimu za umma,serikali za kaunti ,kukosa kuwaajiri walimu na madkatari zaidi ,amekariri pia umuhimu mkubwa uliopo wa nchi kuangalia upya jinsi inavyotumia fedha zake zinazokusanywa kama mapato ya ndani .

Alisema ni wakati mwafaka pia kuangalia kiwango cha mishahara ya maafisa wakuu wa serikali na akaeleza kuwa yuko tayari kupunguziwa mshahara katika jitihada za kuurahisisha mzigo kwa mlipa ushuru.

Kenya ingali inazongwa na madeni makubwa na itahitaji kuangalia kwa umakini matumizi yake ya fedha ili kuafikia malengo yake ya kimaendeleo .

Wataalam wa masuala ya kiuchumi wameafiki kwamba kiasi kikubwa sana cha fedha za umma hupotea kupitiia utumizi mbaya,ufujaji na ufisadi.

Mianya hii mikubwa ndio donda sugu katika utawala wowote na huenda suluhisho la kudumu lisipatikane endapo viongozi wa nchi hawataonyesha nia ya kupambana na maovu hayo kwanza kabla ya kusonga mbele .

Malalamishi ya vijana walioandamana yameifanya nchi kuanza kuyazungumzia mambo hayo .Ushahidi wa mazungumzo haya muhimu ulikuwepo siku ya Jumatano katika bunge la seneti ambapo maseneta walifungua nyoyo kuzungumzia yote haya na yanayohitaji kufanyika ili Kenya kuitumia fursa hii kama funzo na kuweza kujiweka katika mkondo ufaao wa historia .

Iwapo kuna zawadi ambayo vijana wameipa Kenya kupitia maandamano yao ,ni fursa ya kuyazungumza kwa uwazi mambo haya na kuyatafutia ufumbuzi .

Chanzo: www.tanzaniaweb.live