Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maandamano kupinga ukatili wa Vyombo vya Usalama

Sudan Ubakaji Waandamanaji nchini SUdan

Fri, 24 Dec 2021 Chanzo: BBC

Mamia ya wanawake wameandamana nchini Sudan kupinga unyanyasaji wa kingono kufuatia madai kwamba wanawake 13 na wasichana walibakwa katika maandamano ya Jumapili.

Umoja wa Mataifa umesema kuwa umepokea "ripoti za kusikitisha "kwamba maafisa wa Vikosi vya usalama waliwanyanyasa kingono wanawake waliokuwa wakiandamana dhidi ya majeshi.

Marekani na nchi za Magharibi zimekosoa matumizi ya ghasia za kingono "kuwazuia wanawake" kuandamana.

Vikosi vya usalama havijatoa tamko lolote kuhusiana na madai hayo.

Wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika wimbi la maandamano ya kupigania demokrasia ambayo yamekuwa yakifanyika nchini Sudan tangu jeshi lilipofanya mapinduzi mwezi Oktoba.

"Ubakaji hautatuzuia " na "wanawake wa Sudan ni wajasiri" ndio baadhi ya ujumbe uliosheheni maandamano ya Alhamisi katika mji mkuu, Khartoum na Omdurman, kulingana na ripoti za shirika la habari la AFP.

Katika taarifa ya Pamoja, Marekani na Muungano wa Ulaya zililaani ghasia za kingono "kama silaha" ya kuzima sauti ya wanawake.

Taarifa hiyo - ambayo pia ilitiwa saini na Uingereza, Norway, Uswizi na Canada - ilitoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi huru dhidi ya madai ya ghasia.

Watu wawili pia waliripotiwa kuuawa katika maaandamano ya Jumapili, wakati maelfu ya watu waliandamana mjini Khartoum kulaani mapinduzi.

Wanaharakati wanaounga mkono demokrasia wanashutumu jeshi kwa kuiba mapinduzi yaliyosababisha mtawala wa muda mrefu Omar al-Bashir kuondolewa madarakani mwaka 2019.

Kiongozi wa mapinduzi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan ametetea uamuzi wa jeshi wa mwezi Oktoba, kwa madai kuwa jeshi lilichukua hatua hiyo kuzuia vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa sababu makundi ya kisiasa yamekuwa yakichochea raia dhidi ya vikosi vya usalama.

Anasema bado amejitolea kutekeleza mpito kwa utawala wa kiraia, huku uchaguzi ukipangwa kufanyika Julai 2023.

Chini ya makubaliano ya mwezi uliopita yaliyofikiwa na waziri mkuu wa kiraia aliyerejeshwa madarakani Abdalla Hamdok, ataongoza baraza la mawaziri la wanateknolojia hadi uchaguzi ufanyike.

Lakini haijabainika serikali mpya ya kiraia itakuwa na madaraka kiasai gani, kwani itakuwa chini ya uangalizi wa kijeshi.

Kumekuwa na uvumi mkubwa katika siku za hivi majuzi kuhusu mustakabali wa Bw Hamdok, baadhi ya ripoti zikisema kuwa anapanga kujiuzulu huku nyingine zikisema kwamba ameshawishiwa na Jenerali Burhan kusalia madarakani.

Chanzo: BBC