Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maandamano dhidi ya serikali yaendelea kufanyika katika Ethiopia

Maandamano Dhidi Ya Serikali Yaendelea Kufanyika Katika Ethiopia Maandamano dhidi ya serikali yaendelea kufanyika katika Ethiopia

Mon, 10 Apr 2023 Chanzo: Bbc

Maandamano makubwa ya kuipinga serikali yameendelea kufanyika katika jimbo la Amhara nchini Ethiopia yakichochewa na hatua iliyoanzishwa na serikali kuu - ya kuvunja Kikosi Maalum cha Amhara (ASF), kitengo cha kijeshi ambacho kilihusika pakubwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka miwili nchini kaskazini mwa nchi hiyo.

Kumekuwa na maandamano katika takriban miji 12 katika eneo hilo mwishoni mwa juma ambapo waandamanaji walipiga kelele za kukashifu mamlaka. Barabara zimefungwa katika maeneo kadhaa na mawe na matairi yamechomwa ili kuwazuia wanajeshi wa serikali kusafiri ndani na kuingia katika maeneo ya jimbo hilo.

Mapigano kati ya jeshi na ASF yameripotiwa karibu na mji wa Kobo karibu na mpaka na Tigray. Kulingana na kikundi cha utetezi cha Amhara Association of America (AAA) kulikuwa na majeruhi katika mapigano hayo lakini haijatoa takwimu na BBC haikuweza kuthibitisha dai hilo. Huduma za mtandao zimezuiwa katika eneo hilo tangu maandamano yalipozuka.

Kumekuwa na matamshi kadhaa katika siku chache zilizopita huku maandamano yakienea yakiwemo ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed ambaye Jumapili aliapa kuendelea kutekeleza mpango huo "hata iwapo kuna gharama ya kulipwa" na kuonya serikali inaweza kuanzisha "operesheni ya kutekeleza sheria" dhidi ya wanaoizuia.

Mamlaka zinasema kuwa wanachama wa ASF wataunganishwa na jeshi au polisi kuunda kikosi kimoja cha usalama lakini wapinzani katika kanda hiyo wanasema hatua hiyo itaacha eneo hilo kuwa katika hatari ya kushambuliwa na majimbo jirani ya Tigray na Oromia.

Kuna wasiwasi kwamba hii inaweza kusababisha duru mpya ya vurugu baada ya miezi sita ya amani kaskazini mwa Ethiopia- baada ya mkataba wa amani uliotiwa saini mwaka jana.

Chanzo: Bbc