Takriban watu 400 nchini Misri wamekamatwa kutokana na matukio ya ghasia baada ya Rais Abdul Fattah al-Sisi kutangaza kuwa atawania muhula wa tatu, kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo.
Matamshi ya Rais Sisi siku ya Jumanne yalizua ghadhabu ya nadra miongoni mwa umma - video za mitandao ya kijamii zilionyesha maandamano katika mji wa kaskazini-magharibi wa Marsa Matrouh.
Katika picha hizo, watu wanasikika wakiimba "Sisi nje" na kutaka utawala wake wa muongo mmoja uondolewe. Video zingine zilionyesha mapigano kati ya waandamanaji na polisi.
Al -Manassa tovuti kibinafsi ya habari ilimnukuu Saleh Abou-Attiya, katibu mkuu wa Chama cha Wanasheria wa Marsa Matrouh, akisema kuwa watu 400, wengi wao wakiwa "vijana", wamezuiliwa.
Mkuu huyo wa zamani wa jeshi amekuwa madarakani tangu aliposaidia kumuondoa madarakani Mohammed Morsi, kiongozi wa Muslim Brotherhood mwaka 2013 huku kukiwa na maandamano makubwa ya kupinga utawala wake.
Wanaharakati wanasema kuwa muhula wa Bw Sisi madarakani umegubikwa na ukandamizaji wa kikatili wa upinzani na kuporomoka kwa uchumi wa Misri.
Uchaguzi wa rais nchini Misri umepangwa kufanyika mwezi Disemba.