Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maamuzi ya Umoja wa Afrika kuhusu biashara ya binadamu

Pics Pg 17 Okt 08 Maamuzi ya Umoja wa Afrika kuhusu biashara ya binadamu

Fri, 8 Oct 2021 Chanzo: ippmedia.com

KAMISHENI ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Afrika (AU) imeweka sera ya kinga dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu na uhamaji haramu kwa lengo la kupiga vita uvunjifu wa haki za binadamu barani Afrika.

Akizungumza jana katika ufunguzi wa mkutano wa kuthibitisha sera hiyo katika Ukumbi wa Hoteli ya Madinatul Bahri huko Mbweni, Zanzibar, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Dk. Khalid Salum Mohamed, alisema umefika wakati wa kuhakikisha uhalifu huo unapotea Afrika.

Waziri huyo alisema kuwa kwa muda mrefu barani Afrika kumekuwa na matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu kwa kusafirisha watu kwenda nje ya Afrika, jambo ambalo huwaletea madhara makubwa wanapofika ugenini.

Alisema ni jambo lisilopingika kuwa nchi nyingi za Afrika, ikiwamo Tanzania, zinaathirika vibaya kutokana na usafirishaji haramu wa binadamu licha ya kuwapo sheria ya kimataifa inayokataza uhalifu huo.

“Uhalifu huu huwaathiri na kuwakumba zaidi wanawake na watoto na kupelekwa nchi mbalimbali ikiwamo Mashariki ya Kati na hata barani Ulaya ambako hukutana na vitendo mbalimbali vya uvunjifu wa haki za binadamu, ikiwamo mauaji," alisema.

Waziri huyo alisema uthibitishwaji wa sera ya kinga ya usafirishaji haramu wa binadamu na kinga ya uhamaji haramu katika Bara la Afrika ni hatua muhimu na utasaidia katika kuondoa uhalifu huo.

Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Wahamaji (IOM) Tanzania, Qassim Sufi, alisema shirika hilo linatambua madhara ya uhalifu huo ambao kwa kiasi kikubwa husababishwa na hali ya kukosekana kwa amani na utulivu katika baadhi ya mataifa ya Afrika.

Alisema licha ya kuwapo kwa sera hizo, ipo haja kwa kila nchi mwanachama wa AU kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha raia wanalindwa, hasa wanawake na watoto.

Alisema IOM inapenda kuona haki za binadamu zinalindwa hasa kwa wahamaji kwa kuwa ni haki ya kila mwanadamu kuheshimiwa na kupewa haki zake popote duniani.

Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Michezo Utamaduni, Kazi, Ajira na Uhamaji wa AU, Sabelo Mbokazi, alisema Bara la Afrika haliwezi kuwa na amani wala maendeleo ikiwa uhalifu wa kusafirisha binadamu unaendelea kuwapo.

Alisema upatikanaji wa haki za binadamu na uwapo wa sera na sheria madhubuti, utasaidia kuhakikisha raia wa Afrika wanabaki salama katika mataifa yao.

Mkurugenzi huyo alisema utekelezaji wa sera mbili zinazotarajiwa kuthibitishwa katika mkutano huo ni miongoni mwa hatua madhubuti zinazoweza kusaidia katika kutokomeza uhalifu huo barani Afrika.

Hata hivyo, alisema umefika wakati wa kuhakikisha wahalifu wote wanaohusika na uhalifu huo wanafikishwa katika vyombo vya sheria na kufunguliwa mashtaka ili kukomesha vitendo hivyo.

Mkutano huo uliolenga kuthibitisha Sera ya Kinga ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu na Kinga ya Uhamiaji Haramu umehudhuriwa na nchi mbalimbali za AU, zikiwamo Zambia, Algeria, Mauritania na Tanzania.

Chanzo: ippmedia.com