Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini Naledi Pandor ameishutumu idara ya kijasusi ya Israel kwa kujaribu kumtisha kufuatia kesi ya Gaza katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), vyombo vya habari nchini humo vinaripoti.
Bi Pandor Alhamisi aliambia tovuti ya habari ya Mail & Guardian kwamba alikuwa na wasiwasi kuhusu usalama wa familia yake baada ya kulengwa kwenye mitandao ya kijamii..
Waziri huyo alisema alizungumza na Waziri wa Polisi Bheki Cele kuhusu kuimarisha usalama wake baada ya kupokea ujumbe wa vitisho.
"Maajenti wa Israeli, idara za kijasusi, [hivi] ndivyo wanavyofanya, na wanatafuta kukutisha, kwa hivyo ni lazima tusitishwe. Kuna kitu kinachoendelea," alinukuliwa akisema.
Israel bado haijatoa maoni yoyote kuhusu matamshi ya waziri huyo.
Mwezi uliopita, ICJ iliiagiza Israel kuchukua hatua za kuzuia mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina huko Gaza na kutoa ripoti ndani ya mwezi mmoja.
Afrika Kusini ilikuwa imewasilisha kesi dhidi ya Israel katika mahakama hiyo kuhusu madai ya ukiukaji wa haki za binadamu uliofanywa na Israel katika mzozo huo.
Bi Pandor alisema serikali imeazimia kuona kesi ya ICJ ikikamilika.
Maoni yake yanakuja siku chache baada ya Rais Cyril Ramaphosa kuzungumza juu ya uwezekano wa kampeni ya kupigana dhidi ya Afrika Kusini baada ya uamuzi wa ICJ.