Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘MO’ awa bilionea wa 13 Afrika, amshukuru JPM kwa uwekezaji

0c2327e88f4ac93ef727b209ecea1cba ‘MO’ awa bilionea wa 13 Afrika, amshukuru JPM kwa uwekezaji

Mon, 25 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MFANYABIASHARA maarufu nchini Mohammed Dewji ‘MO’ (pichani) ambaye jana Jarida la Forbes lilimtamka kama bilionea namba 13 barani Afrika, ameshukuru serikali ya Rais John Magufuli kwa kuweka mazingira ya uwekezaji vyema na hivyo kuruhusu shughuli za kiuchumi kufanyika kwa ufanisi zaidi.

Anashikilia nafasi hiyo akiwa na utajiri wa dola za Marekani bilioni 1.6. Alisema kupanda kwake kutoka nafasi ya 16 kwa mwaka uliopita na kufikia wa 13 kunatokana na mazingira bora ya uwekezaji yaliyomfanya kuendelea kupaa katika medani za biashara na viwanda, hivyo anaishukuru serikali kwa kuendelea kuwezesha wawekezaji kusonga mbele, wakitengeneza bidhaa na ajira.

Alisema mazingira mazuri hayo yamemwezesha hadi sasa kuajiri watu zaidi ya 35,000 katika shughuli zake mbalimbali nchini na kwamba ifikapo mwaka 2025 atakuwa amewezesha ajira kwa watu 100,000.

Dewji amewekeza katika maeneo mbalimbali yakiwemo vinywaji baridi, ngano na pia katika mashamba makubwa ikiwamo mkonge. Pamoja na kupata nafasi hiyo ya 13 akiwa na umri wa miaka 45 amebaki kuwa bilionea kijana.

Mwaka jana alikuwa wa 16 na bilionea kijana. Kwa mujibu wa Forbes kwa miaka 6 amekuwa bilionea kijana Afrika. “Nashukuru serikali ya awamu ya tano kwa kubadili mazingira ya uwekezaji mpaka nimepaa katika nafasi niliyoshika mwaka jana.

Maendeleo haya yamewezekana kwa sababu ya mabadiliko makubwa katika mazingira ya uwekezaji nchini yanayotoa fursa kwa wawekezaji kufanya vyema,” alisema Mo katika mahojiano.

Aidha alisema kwamba pamoja na kuwa tajiri , ataugawa utajiri wake kwa wenye mahitaji awe hai au amefariki dunia. Katika ripoti hiyo ya Forbes mfanyabiashara tajiri nchini Nigeria, Aliko Dangote ameorodheshwa kwa mara ya 10 mfululizo, kuwa mtu tajiri zaidi barani Afrika, akishika namba moja .

Dangote mwenye umri wa miaka 63 anafanya biashara ya saruji, sukari na ana utajiri wa dola Bilioni 12.1. Wengine katika orodha hiyo ni Nassef Sawiris mwenye utajiri wa dola za Marekani bilioni 8.5 akijishughulisha na uwekezaji na ujenzi; Nicky Oppenheimer ni wa tatu akiwa na utajiri wa dola za Marekani bilioni 8 akijishughulisha na biashara ya almasi; Johann Rupert yeye ana utajiri wa dola za Marekani bilioni 7.2 na amewekeza kwenye biashara za anasa; Yupo Mike Adenuga mwenye utajiri wa dola za Marekani 6.3 akiwa anashughulika na biashara za mafuta na simu na Abdulsamad Rabiu mwenye utajiri wa dola za Marekani 5.5 akijishughulisha na saruji na sukari.

Wengine na utajiri wao katika kipimo cha dola za Marekani katika mabano ni Issad Rebrab ( bilioni 4.8); Naguib Sawiris (Bilioni3.2); Patrice Motsepe (bilioni 3);Koos Bekker (bilioni 2.8); Mohamed Mansour (Bilioni 2.5); Aziz Akhannouch (bilioni 2) na wa 14 ni Youssef Mansour ( Bilioni 1.5).

Wengine ni Othman Benjelloun (bilioni 1.3);Michiel Le Roux (bilioni 1.2);Strive Masiyiwa (bilioni 1.2) na Yasseen Mansour (bilioni1.1). Mwaka jana Mo Dewji alishika nafasi ya 16 ya mabilionea Afrika licha ya utajiri wake kupungua kwa Dola milioni 300 (Sh 692.67 bilioni).

Katika orodha ya jarida hilo mwaka juzi Mo ambaye anayefanya biashara mchanganyiko alikuwa nafasi ya 14 akiwa na utajiri wa Dola bilioni 1.9 (Sh4.3trilioni) .

Kufikia nafasi ya 13 mwaka huu maana yake bilionea huyo amepanda kwa nafasi tatu kutoka 16 ya mwaka jana. Mo Dewji aliyezaliwa Mei 8, 1975 huko Ipembe, Singida maeneo ya katikati mwa Tanzania,alisomea elimu ya msingi katika shule ya msingi ya Arusha na baadaye akasomea elimu ya sekondari katika Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST) jijini Dar es Salaam.

Baadae alisoma masomo ya sekondari nchini Marekani jimbo la Florida mwaka 1992. Alisomea chuo kikuu cha Gergetown jijini Washington DC na kuhitimu mwaka 1998 akiwa na shahada ya kwanza katika biashara ya kimataifa na fedha, na masuala pia ya dini.

Miongoni mwa watu mashuhuri waliosomea chuo kikuu hicho ni rais Bill Clinton, rais wa zamani wa Ufilipino Gloria Arroyo, Mfalme wa Jordan Abdullah na wachezaji wa NBA kama vile Allen Iverson na Patrick Ewing. Baada ya kufuzu, alirejea Tanzania na kuanza kushiriki katika usimamizi wa kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL) iliyoanzishwa na babake miaka ya 1970.

Chanzo: habarileo.co.tz