Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAAJABU: Wajua kama Franco alizikwa mara mbili?-1

89686 Franco+pic MAAJABU: Wajua kama Franco alizikwa mara mbili?-1

Tue, 24 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Rekodi ambayo haiwezi kusahaulika barani Afrika pengine duniani kote, ni ya aliyekuwa mwanamuziki nguli Hayati Franco Luambo Makiadi, mwili wake kuzikwa mara mbili kwa nyakati na makaburi tofauti.

Tukio jingine ni lile ambalo kamwe halijasikika sehemu nyingine ni lile la mke mmoja kuolewa na marais wawili kwa nyakati tofauti.

Graca alikuwa mke wa Rais wa Msumbiji hayati Samora Machael. Baada ya kufariki mumewe, akaolewa na aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Hayati Nelson Mandela ‘Mzee Madiba’.

Wapenzi na mashabiki wa muziki wa dansi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), na nchi jirani, kila mwaka ifikapo mwezi wa Oktoba hufanya kumbukizi ya kifo cha mwanamuziki Franco Luambo Makiadi.

Alifikwa na mauti akiwa katika hospitali moja kule Ubelgiji, alikokuwa amelazwa kwa matibabu ya maradhi yaliyomsumbua kwa muda mrefu.

Baada ya kutokea kifo hicho, mwili wake ulisafirishwa kurejeshwa kwao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Zaire zamani), kwa ajili ya mazishi.

Jeneza lililobeba mwili wa Franco, lilipitishwa mitaani kuagwa na wananchi huku, likisindikizwa na ulinzi mkali wa polisi. Wakati huohuo serikali ikatangaza siku nne za maombolezo ya kitaifa.

Wakati wa uhai wake Francois Lokanga la Djo Pene Luambo Makiadi, alikuwa akiishi Mtaa wa Kasa Vubu, jijini Kinshasa.

Mazishi ya kwanza

Lwambo Makiadi alifariki mwaka Oktoba 12, 1989 na mazishi yake yalifanywa kuwa ya kiserikali. Alipewa heshima zote za kitaifa chini ya Serikali ya Rais Mobutu Seseseko Kuku Ngíendu Wazabanga.

Viongozi na wawakilishi mbalimbali kutoka nchi za Kiafrika na mamia kwa maelfu ya Wazaire, walijumuika katika Jiji la Kinshasa kutoa heshima zao za mwisho kwa Franco.

Siku ya mazishi yake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Leon Kengo wa Dondo, alikwenda kutoa heshima za mwisho kwa niaba ya serekali.

Wakati wa misa maalumu ya mazishi, Padri alitamka “Luambo alikuwa Mtume wa muziki, hakuna alichokisahau katika utunzi wake, kavichambua vitu kadhalika na watu wa kila rika, hata Rais Mobutu hajaachwa nyuma.

“Nyimbo zake kadhaa zilipigwa marufuku, hata hivyo ziliendelea kupendwa sana na umma. Nyimbo zake nyingine hadi leo huchukuliwa kama nembo ya taifa,” alitamka Padri huyo.

Katika siku za maombolezo Radio ya Taifa hilo ilikuwa ikipiga nyimbo za Franco hadi Oktoba 17, 1989 alipowekwa kwenye nyumba yake ya milele.

Mazishi ya pili

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, aliyafukua mabaki ya mwili wa Franco Luanzo Makiadi, yaliyokuwa katika Makaburi ya Gombe yakapelekwa kwenda kuzikwa kwa mara ya pili kwenye makaburi mapya ya Kinkole.

Makaburi hayo yapo karibu na Nsele, nje kidogo ya Jiji la Kinshasa huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Kwa kuthamini mchango wake mkubwa kwa taifa, Waziri Mkuu, Augustine Matata kwa niaba ya serikali, alizindua mnara wa Luambo Franco Oktoba 17, 2015 wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 26 ya kifo chake zilizofanyika katika Jiji la Kinshasa.

Hatua hiyo ya serikali ni kuthamini kazi nzuri alizozifanya mwanamuziki huyo za kuelimisha, kuburudisha na kuhamasisha maendeleo ya nchi sanjari na kuinua uchumi wa nchi hiyo kupitia tasnia ya muziki.

Aidha serikali ilimpa heshima Franco Luambo Makiadi kwa kubadilisha jina la Barabara ya Jean Bendel Bokassa Avenue kuwa Lwambo Makiadi Avenue.

Bokassa alikuwa rais wa nchi ya Afrika ya Kati, pia alikuwa chanda na pete wa Rais Mobutu Seseseko.

Chini ya uongozi wa Rais Joseph Kabila, serikali yake iliazimia kujenga studio kubwa ya kurekodi muziki na kupewa jina la mwanamuziki huyo maarufu barani Afrika na duniani.

Aidha hatua nyingine zilizoazimiwa na serikali hiyo za kumuenzi Franco Makiadi, ni kujenga Jumba la Makumbusho ambako kumewekwa vitu vyote alivyokuwa akitumia hayati Franco Makiadi enzi za uhai wake.

Vitu hivyo ni pamoja na magitaa yake likiwemo lile la galaton, aliloanzia kujifunza kupiga gitaa, gari alilokuwa akilitumia, viatu pamoja na nguo alizokuwa akizivaa.

Katika sherehe hizo ilitamkwa serikali itaendelea kuwaenzi wasanii wote. Iliahidi kujenga minara ya nguli wengine waliotangulia mbele za haki akiwemo Tabu Ley, Joseph Kabasele ‘Grand Kale’ Papa Wemba na wengine.

Wasifu wa Franco:

Franco alikuwa akijulikana kwa majina ya Luambo Makiadi Lokanga La Dju Pene Francois, maarufu kama Franco Yogo.

Alizaliwa Julai 06, 1938, katika Kijiji cha Sona Bata Magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Akiwa bado mdogo, wazazi wake walihamia Jiji la Leopodville (sasa Kinshasa).

Baba yake Joseph Emongo alikuwa mfanyakazi wa shirika la reli na mama yake alikuwa akioka na kuuza mikate sokoni.

Mwanamuziki maarufu Paul Ebengo Dewayon ndiye aliyegundua kipaji cha mtoto huyu, akaanza kumfundisha rasmi namna ya kupiga gitaa.

Akiwa na miaka 15 alirekodi wimbo wake wa kwanza wa Bolingo na ngai na Beatrice (Mapenzi yangu kwa Beatrice).

Wimbo huo aliutunga alipojiunga na bendi iliyokuwa inamilikiwa na Studio za Loningisa.

Kiongozi wa bendi hiyo Henri Bowane ndiye aliyeanza kufupisha jina la mwanamuziki huyu la FranÁois akamuita Franco, jina alilokuja kujulikana nalo maisha yake yote.

Serikali ya Zaire wakati huo ilimtunuku heshima ya Grande Maitre, ambayo ilikuwa mahsusi kwa Majaji na Wasomi.

Mwaka 1955 alianzisha bendi akishirikiana na Jean Serge Essous, iliyozinduliwa katika Ukumbi wa Bar ya OK. Baadaye wakaipa jina la Tout Puissant OK Jazz (T.P.OK Jazz).

Katika kipindi kifupi Franco akiwa na mwimbaji Vicky Longomba (Baba yake Lovy na Awilo Longomba), walianza kuwa wapinzani wakubwa wa bendi ya African Jazz, iliyokuwa ikiongozwa na Joseph Kabasele ‘Grand Kalle’.

Chanzo: mwananchi.co.tz