Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

M23: Makubaliano ya DRC na Rwanda hayatuhusu

M23 Sultan.png M23: Makubaliano ya DRC na Rwanda hayatuhusu

Fri, 8 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kundi la waasi wa M23 linaloendesha harakati zake mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limesema halitaheshimu wala kufungamana na makubaliano ya usitishaji vita yaliyoafikiwa Jumatano baina ya viongozi wa DRC na Rwanda.

Msemaji wa M23, Willy Ngoma ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, makubaliano hayo yaliyofikiwa kufuatia mazungumzo ya siku moja yaliyofanywa na marais wa nchi hizo mbili kwa upatanishi wa rais wa Angola hayana umuhimu wowote.

Ngoma amebainisha kuwa, "Sisi ni Wakongomani, na wala si Wanyarwanda. Mapatano yoyote ya usitishaji vita yanapaswa kuwa baina yetu na serikali ya DRC."

Kufuatia mazungumzo ya marais Felix Tshisekedi wa Kongo DR na Paul Kagame wa Rwanda yaliyofanyika kwa upatanishi wa Rais Joao Lourenco mjini Luanda Jumatano, pande hizo mbili zimetolewa mwito wa kurejesha katika hali ya kawaida uhusiano wao wa kidiplomasia, kukomesha uhasama uliopo na "kuondoka mara moja na bila masharti yoyote" wanamgambo wa M23 katika maeneo walipo mashariki ya DRC.

Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimekuwa zikishambuliana kwa maneno baada ya DRC kudai kwamba, serikali ya Kigali inawaunga mkono waasi wa M23 wa nchini Kongo ambao akthari ya wapiganaji wake wanatoka kabila la Tutsi.

Rwanda nayo inaituhumu DRC kuwa inaliunga mkono kundi la waasi ambalo baadhi ya wanachama wake walihusika katika mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini Rwanda mwaka 1994. Kila nchi inazikanusha tuhuma zilizoelekezwa dhidi yake.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live