Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

M23: Hii ni ishara ya nia njema iliyotolewa kwa niaba ya amani

Waasi Wa M23 Waunga Mkono Harakati Za Kuleta Amani DR Congo M23: Hii ni ishara ya nia njema iliyotolewa kwa niaba ya amani

Mon, 26 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Hatimaye kundi la waasi la M23, ambao wameteka maeneo mengi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wameahidi kujiondoa na kuonyesha dalili za kwanza za amani na utulivu kwa raia.

Kwa mujibu wa kituo cha habari Daily Nation, wameeleza waasi hao walitangaza kujiondoa kwenye nafasi yao katika mji wa Kibumba, takribani kilomita 20 kutoka Goma, sehemu ambayo ni kitovu cha kibiashara cha zaidi ya watu milioni moja.

Tangu kuanzishwa tena kwa mashambulizi yake Oktoba, waasi wa M23, wengi wao kutoka jamii ya Watutsi, wamedhibiti maeneo makubwa ya mkoa wa Kivu Kaskazini, unaopakana na Rwanda na kusababisha kuongezeka mvutano kati ya mataifa hayo mawili.

Kundi hilo liliombwa kuondoka katika maeneo hayo, ambapo walisema kuwa wanajiandaa kujiondoa na kuachia eneo la Jeshi la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACRF), ambalo lilitumwa mwezi uliopita ili kufanikisha suala la amani kwa kusitisha mapigano.

Katika taarifa yao, M23 walisema wanakabidhi sehemu hiyo ya nchi kwa EACRF kama ishara ya nia njema, ambayo ni sehemu ya mapendekezo ya mkutano mdogo wa wakuu wa nchi uliofanyika Luanda, Angola Novemba 23, 2022.

Msemaji wa kisiasa wa kundi hilo, Lawrence Kanyuka aliyetia saini taarifa hiyo aliongeza: “Tumaini letu ni kuwa Serikali ya Kinshasa itaipokea taarifa hii kwa mikono miwili na pia kujitahidi kuleta amani katika nchi yetu.

Katika hafla ya kujiondoa siku ya Ijumaa, Desemba 23, 2022 mjini Kibumba, Kamanda wa kikosi cha Kanda ya Afrika Mashariki, Meja Jenerali Jeff Nyagah alitoa wito kwa raia waliokimbia eneo hilo kurejea kwa sababu sasa lipo salama.

“Tumejitolea kufanya operesheni kwa mujibu wa sheria za kibinadamu na kimataifa. Tunafahamu utata wa eneo la operesheni, lakini bidii na dhamira yetu iko sawa,” alisema Jenerali Nyagah.

M23 wamefikia hatua hiyo kufuatia mahitimisho ya mikutano iliyofanywa na EACRF, ikiwa ni siku kadhaa baada ya kutolewa ripoti mpya ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa inayolishutumu jeshi la Rwanda kwa kuendesha operesheni za kijeshi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na kusambaza silaha, risasi na sare kwa waasi hao.

Chanzo: Mwananchi