Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lifahamu kundi la waasi ADF kutoka Uganda linaloshirikiana na Islamic State

SfdGSHDF Lifahamu kundi la waasi ADF kutoka Uganda linaloshirikiana na Islamic State

Wed, 17 Nov 2021 Chanzo: BBC

Eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kwa muda mrefu limekuwa ngome ya shughuli za waasi ambapo mizozo hiyo husambaa hadi nchi majirani za Rwanda, Burundi na Uganda.

Kati ya makundi yenye sifa mbaya zaidi yanayoendesha shughuli zao huko ni lile la kutoka nchini Uganda la Allied Democratic Forces (ADF).

Kundi hilo la Kiislamu liliundwa miaka ya 1990 na mara nyingi lilihusika na mizozo ya ndani na taifa la Uganda. Lakini baada ya kuibuka nchini DR Congo, shughuli zake zemechukua mkondo wa kundi la jihadi huku mashambulizi yake mengi yakidaiwa kutekekelezwa kwa jina la kundi la Islamic State (IS).

Ni kwa namna gani waasi wa Uganda walikuwa washirika wa IS? Kwanini usalama bado ni changamoto DRC? Washambuliaji wa kujitoa mhanga jana Jumanne waliulenga mji mkuu wa Uganda Kampala, na kuua takriban watu sita na kujeruhi wengine zaidi ya 30. IS ilitoa taarifa kwenye kituo chake cha Telegram, kisha kuripotiwa na Shirika lake la Habari la Amaq, ikisema kwamba wanachama wake walifanya mashambulizi hayo.

Maafisa walikuwa wamelilaumu kundi la Allied Democratic Forces (ADF), kundi la waasi ambalo liliahidi utiifu wake kwa IS mwaka 2019.

ADF ilianza vipi? ADF lilianzishwa kaskazini mwa Uganda na maafisa wa zamani wa jeshi watiifu kwa aliyekuwa rais wa Uganda Idi Amin. Likachukua silaha dhidi ya rais wa muda mrefu nchini Uganda Yoweri Museveni likidai kuwa serikali ilikuwa inaendesha mateso dhidi ya Waislamu.

Video ya wanamgambo wa IS baada ya shambulio katika kijiji kimoja kwenye jimbo la Ituri

Baada ya kushindwa na jeshi la Uganda mwaka 2001 lilihamia mkoa wa Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Kufuatia kipindi cha kutokuwa na shughuli nyingi, ADF lilibuka tena mwaka 2014 kwa kendesha misururu ya mashambulizi dhidi ya raia nchini DRC.

Musa Seka Baluku akawa kiongozi mwaka 2015 kufuatia kukamatwa kwa mtangulizi wake Jamil Mukulu. Bakulu anaripotiwa kutangaza kulitii kundi la IS kwanza mwaka 2016.

Lakini ni hadi Aprili mwaka 2019 ndiposa IS walikiri kuendesha shughuli eneo hilo, wakati lilidai kuhusika kwenye shambulizi dhidi ya vituo vya jeshi karibu na mpaka wa Uganda. Taarifa hii ndiyo ilitangaza kile kinachofahamika kama IS Central Africa Provinc (Iscap), ambayo ilikuja kujumuisha hadi Msumbuji.

Licha ya kuwepo ishara kuwa IS wameungana na ADF, IS haijalitamka hadharani kundi hilo kwenye propaganda zake. Septemba 2020 , Baluku alidai kuwa ADF halipo tena.

"Kwa sasa sisi ni mkoa, mkoa wa Afrika ya kati, ambao ni mmoja wa mikoa mingi ambayo inaunda Islamic State," alisema.

Hali iko vipi nchini DR Congo? Kulingana na shirika la kuwahudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR. ADF imewaua mamia ya raia na kuwalazimu zaidi ya watu 40,000 kuhama eneo la Beni tangu Januari mwaka 2021. Kundi hilo la waasi pia linawalenga wanajeshi wa serikali na wale wa UN.

Tangu IS iibuke nchini DR Congo, mashambulizi yameongezeka.

Mashambulizi ya Iscap yanatokea katika himaya ya ADF, eneo la Beni lililo Kivu Kaskazini pia yakiwemo mashambulizi wakati mwingine kwenda mkoa jirani wa Ituri.

Shughuli za ADF zimejikita zaidi katika eneo la Beni, Kivu Kaskazini

Mengi ya mashambulizi haya hulenga kambi za jeshi, lakini mabaya zaidi ni dhidi ya raia Wakisristo. Shambulizi kubwa zaidi la Iscap linatajwa kuwa la Oktoba 2020 kwenye gereza mjin Beni, lililosababisha zaidi ya wafungwa 1,000 kutoroka.

Hofu ya mzozo wa kidini Mzozo uliopo Mashariki mwa DR Congo wakati mwingi umechochea misukosuko ya kidini lakini kuhusika kwa IS huenda kukachochea zaidi. DR Congo ni nchi yenye waumini wengi wa kanisa katoliki na kanisa lina nafasi kubwa nchini humo. Waislamu huchukua asilimia 10.

Jamii ya Waislamu huko Beni hulipinga kundi hili lakini pia inakuja na gharama zake. Mwezi Mei makasisi wawili maarufu waliokuwa wakosoaji wa ADF waliuawa huko Beni. Kundi hilo la waasi pia limehusishwa na mashambulizi dhidi ya waumini wa katoliki. Mwezi Oktoba mwaka 2012 liliwateka maaskofu watatu wa kanisa Katoliki eneo la Mbau.

Kwenye propaganda zake IS, imewalenga Wakiristo na kuikejeli serikali ya DR Congo kwa kushindwa kuwalinda kutoka kwa mashambulizi yake.

Propaganda za IS ADF haionekani kumiliki vyombo vyake vya habari au kudai kuhusika kwenye mashambulizi. Lakini IS ina mifumo yake ya mitandaoni. Nyingi ya propaganda za Iscap zinahusu madai yaliyoandikwa ya kuhusika kwenye mashambulizi na picha za matokeo yake.

Propaganda za Iscap zimejumuisha pia picha za watoto

Mwezi Machi kama njia ya kuonyesha ubabe wake, Iscap ilitoa picha zilizodaiwa kuonyesha wapiganaji wake wakirandaranda katika kijiji kimoja mkoa wa Ituri kufuatia shambulizi dhidi ya jeshi. Lakini picha kama hizo ni adimu na ni ishara kuwa bado IS halijakita mzizi nchini DR Congo.

Kusambaa kwa makundi ya Jihad Ghasia zinazoendeshwa na waasi nchini DR Congo zimechangiwa kutokuwepo serikali dhabiti na kutoamini hatua za jeshi.

Haya ndiyo mazingira ambapo IS inaweza kusambaa kama ilivyokuwa nchini Iraq na Syria mwaka 2014 na hivi karibuni eneo la Afrika magharibi ambapo imesambaa kuanzia Kaskazini Mashariki mwa Nigeria hadi eno la Sahel.

Iscap huenda ikatumia hali ya kuongezeka ghasia kuweza kusambaa kwenda nchi majirani.

Chanzo: BBC