Mkuu wa Baraza la Mpito la Kijeshi la Chad ameonana na Mkuu wa Baraza la Uongozi la Libya na pande mbili zimefikia makubaliano ya kushirikiana kulinda usalama katika maeneo tofauti ya mpakani ya nchi hizo mbili ili kulinda usalama wa raia.
Magenge ya waasi yamepanua wigo wa mashambulio yao kutoka Nigeria hadi katika nchi za Niger, Chad na Cameroon na kutishia usalama wa nchi nyingine zinazopakana na nchi hizo nne ikiwemo Libya.
Shirika la habari la ISNA leo Jumatatu limenukuu taarifa ya Ikulu ya Rais wa Chad na kusema kuwa, Mahamat Idriss Déby Itno, Mkuu wa Baraza la Mpito la Kijeshi la Chad amekutana na Mohammed al Menfi, Mkuu wa Baraza la Uongozi la Libya na wamejediliana namna ya kudhamini usalama katika maeneo ya mpakani ya nchi hizo mbili.
Mazungumzo ya Déby na al Menfi yamefanyika pambizoni mwa kikao cha dharura cha Umoja wa Afrika huko Malabo, mji mkuu wa Guinea ya Ikweta.
Katika mazungumzo hayo, pande hizo mbili zimetilia mkazo wajibu wa kushirikiana kukomesha migogoro iliyopo kama magendo ya silaha katika maeneo ya mpakani na pia kuwa na uratibu wa pamoja wa kulinda usalama wa maeneo hayo.
Hayo yameripotiwa siku kadhaa baada ya vyombo vya habari vya Chad kuripoti taarifa ya kutokea mapigano ya umwagaji wa damu kati ya magenge yenye silaha ya Chad katika mpaka wa nchi hiyo na Libya karibu na migodi ya dhahabu.
Kukosekana serikali kuu yenye nguvu nchini Libya ni tatizo jingine linalosababisha ukosefu wa usalama ambao unawafanya viongozi wa nchi jirani ikiwemo Chad kuwa na wasiwasi mkubwa.