Nchini Liberia, Jaji Mkuu wa zamani Gloria Musu Scott pamoja na watu watatu wa familia yake wamefungwa jela maisha kwa kosa la kutekeleza mauaji.
Wanne hao walikamatwa na kufunguliwa mashtaka mwezi Juni mwaka jana kwa kuhusishwa na kifo cha Charlotte Musu, ambaye aliripotiwa kuwa mpwa wa Scott.
Mwezi Februari mwaka uliopita, Charlotte aliuawa na watu wasiojulikana katika makazi ya Scott katika mji wa Brewerville, Kaskazini –Magharibi wa Liberia.
Jaji huyo mkuu wa zamani awali alikuwa amesisitiza kwamba watu wasiojulikana walivamia makazi yake ambapo walitekeleza mauaji ya mpwa wake.
Baada ya miezi minne ya kusikilizwa kwa kesi hiyo Mahakamani katika mji mkuu wa Monrovia, mwezi uliopita walipatikana na kosa la kumuua Charlotte.
Wanawake hao wanne pia walipatwa na kosa na kupanga na kutoa taarifa na ilani ya uongo kwa maofisa wa polisi.
Katika kipindi chote cha kusikilizwa kwa kesi dhidi yao, watuhumiwa walisisitiza kutokuwa na kosa kama walivyoshtakiwa.
Mahakama imesema ilipata ushahidi wa kutosha kufunga jela wahusika kwa mauaji hayo.
Liberia ilitupilia mbali adhabu ya kifo mwezi Juni mwaka uliopita.
Mawakili wa Scott tayari wamesema watakata rufa kupinga uamuzi huo wa mahakama.
Alihudumu katika nafasi ya Jaji Mkuu wa Liberia kati ya mwaka 1997 hadi 2003.