Mapinduzi ya kijeshi nchini Niger yamezua hali ya wasiwasi miongoni mwa nchi jirani katika eneo la Sahel. Sababu kuu ya wasiwasi huu mkubwa ni kwamba ukosefu wa utulivu umeongezeka katika Sahel, jiografia inayoanzia Bahari ya Atlantiki hadi Bahari ya Shamu.
Kabla ya Niger, eneo hilo la Sahel limeshuhudia mapinduzi mengine ya kijeshi yaliyofanyika katika nchi za Burkina Faso na Mali katika miaka mitatu iliyopita.
Lakini hali ya Niger siyo tu kwamba inatia wasiwasi eneo la Sahel, inaweza pia kuwa na athari kubwa duniani kote. Kuongezeka kwa ghasia
Niger ilikuwa moja ya nchi zenye demokrasia adimu ambayo hata nchi za Magharibi ziliiona kama yenye hali tulivu katika eneo hilo ambapo mashambulizi ya kikatili yameongezeka hivi karibuni. Hata hivyo, kuna wasiwasi kwamba utulivu huu unaweza kuvurugika kutokana na mapinduzi ya kijeshi.
Nchi hiyo ina kambi za kijeshi za Ufaransa na Marekani zinazopigana dhidi ya Boko Haram na makundi ya kijihadi yenye mahusiano na ISIS.
Mustakabali wa kambi hizi haujulikani kwa sasa. Mapinduzi ya kijeshi nchini Mali na Burkina Faso yalisababisha ongezeko la mashambulizi ya kikatili yanayofanywa na makundi yenye itikadi kali.
Pia inazua wasiwasi kwamba Niger inaweza pia kuwa mahala pa kuwavutia makundi haya.
Utamaduni wa mapinduzi kushamiri
Pamoja na mapinduzi ya Niger, sehemu ya Afrika inayoanzia Mali magharibi hadi Sudan mashariki sasa iko chini ya udhibiti wa tawala za kijeshi.
Kuongezeka kwa tawala za kimabavu katika eneo la Sahel kunamaanisha kurudisha nyuma demokrasia ya eneo hilo. Mapinduzi nchini Niger pia yanaweza kuhamasisha vitengo vya kijeshi katika nchi nyingine kunyakua mamlaka.
Wasiwasi huu pia unaeleza vyema kwa nini jumuiya ya kiuchumi ya ECOWAS iliamua kwamba itaiwekea vikwazo serikali ya kijeshi ikiwa Rais Bazum hatarejeshwa maamlakani. Hatua hii inaungwa mkono na Marekani, Umoja wa Ulaya (EU) na Umoja wa Mataifa.
Baada ya mapinduzi ya Mali na Burkina Faso, serikali za nchi zote mbili zilidumisha ushirikiano wa karibu na Urusi. Jeshi nchini Niger linatoa hisia kwamba linaweza kuelekea upande huo huo.
Hakuna ushahidi wa kuhusika kwa Urusi katika mapinduzi ya kijeshi nchini Niger. Msemaji wa Kremlin alitaka pia kuachiliwa kwa Bazum na suluhisho la amani kwa mzozo huo.
Hata hivyo, wachambuzi wa kisiasa wanaounga mkono Kremlin walisifu mapinduzi hayo katika vituo vya habari vinavyofadhiliwa na serikali na kupitia akaunt za Telegram. Waandamanaji waliounga mkono mapinduzi hayo walipeperusha bendera za Urusi na kulaani ukoloni wa zamani wa Ufaransa. Pia kuna wasiwasi kwamba kundi la mamluki la Urusi Wagner linapanua ushawishi wake nchini Niger.
Ikiwa Niger itafuata nyayo za majirani zake, haswa kundi la Wagner, hii inaweza kusababisha kuongezeka kwa ghasia, ukiukwaji wa haki za binadamu na ukwapuaji wa madini.
Madini ya Urani (Uraniam)
Niger ina karibu asilimia tano ya usambazaji wa kimataifa wa radioactive metal element uranium, ambayo inaundwa na madini ya Urani na hutumiwa katika nishati ya nyuklia. Niger ilikuwa muuzaji mkubwa wa pili wa madini asilia ya Urani huko EU mwaka jana, kulingana na wakala wa nyuklia wa Umoja wa Ulaya EURATOM. Aidha, nchi hiyo inakidhi takriban asilimia 15 ya mahitaji ya urani ya Ufaransa.
EURATOM inasema kuwa hakuna hatari ya haraka kwa uzalishaji wa nishati ya nyuklia barani Ulaya ikiwa Niger itapunguza usambazaji wake wa madini hayo. Kwa sababu mitambo ya nguvu za nyuklia inaweza kuendelea kwa miaka mitatu ijayo bila kutegemea Urani ya Niger.
Licha ya hayo, ECOWAS au washirika wake wa Magharibi hawataki Urani ambayo inatumika kiraia na kijeshi, kuangukia katika mikono isiyo sahihi katika maeneo ambayo wanamgambo wa Kiislamu wenye itikadi kali wanafanya kazi na Wagner hilo linaweza kupanua nyanja yake ya ushawishi.
Serikali ya Bazum inashirikiana na nchi za Ulaya katika kuzuia msururu wa wahamiaji kupitia Bahari ya Mediterania na kuwahifadhi mamia ya wakimbizi katika vituo vya kizuizini nchini Libya.
Wakati huo huo, Bazum pia alichukua hatua dhidi ya wasafirishaji haramu wa binadamu nchini humo, nchi ambayo ni kivuko muhimu kati ya nchi za Afrika Magharibi na nchi za kaskazini.
Lakini chini ya mamlaka ya kijeshi, ahadi hizi zinaweza kuwa za kutiliwa shaka, hasa baada ya baadhi ya washirika wa Ulaya kama vile Ufaransa na Uingereza kusema kuwa watasitisha misaada kwa Niger.
Hii inaweza kuwa na athari kubwa kwa suala la wahamiaji kwenda Ulaya. Linaweza kuongeza idadi ya wahamiaji wanaotokea eneo hilo kwenda Ulaya.