Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kundi la wanawake 60 latembea kilometa 300 kwa siku 9 kwenda kumuona Papa Francis

Kundi Kundi la wanawake 60 latembea kilometa 300 kwa siku 9 kwenda kumuona Papa Francis

Sat, 4 Feb 2023 Chanzo: Bbc

Kundi la takribani mahujaji 60 wa Kikatoliki wanapata ahueni baada ya kutumia siku tisa wakitembea Sudan Kusini iliyokumbwa na vita ili kumwona Papa Francis katika mji mkuu wa Juba.

"Miguu yangu inauma, lakini sijachoka sana. Roho inapokuwa na wewe, huchoki," NightRose Falea alisema huku akiilamba midomo yake iliyopasuka na mikavu.

"Nisingekosa kuja Juba kwa vyovyote vile. Tuko hapa kupata baraka za Papa. Nina imani kuwa kwa baraka zake mambo yatabadilika katika nchi hii," aliambia BBC.

Wakiongozwa na imani na hisia za uzalendo, wanawake hao wametoka Rumbek - kama kilomita 300 (maili 190) kaskazini-magharibi mwa Juba.

Dhamira yao ikiwa ni kuungana na Papa katika kuliombea taifa hilo changa zaidi duniani, ambalo limekumbwa na migogoro tangu lilipopata uhuru wake mwaka 2011 - hali ambayo imeleta masaibu makubwa kwa mamilioni ya watu wake.

"Tulitembea kwa saa kadhaa kila siku na kisha tukalala kwenye parokia za njiani. Ilikuwa ya kuchosha lakini inafaa," alisema Faith Biel.

Walipokuwa wakitembea kwa maili chache zilizopita, vumbi na nyimbo za shangwe zilisikika huku msafara wa watu ukiimba na kukanyaga miguu yao.

Shangwe hizo zilivutia umati wa watazamaji. Wengine walijiunganao kucheza. Wengine, bila uhakika, walisimama kwa umbali ili kutoa nafasi kwa kundi hilo la wanawake waliovalia nguo nyeupe na kuvaa hijabu zenye alama ya uso wa Papa.

Nguo zao zilizochafuka, miguu yenye malengelenge na midomo iliyopasuka ilithibitisha mateso ya safari ya siku tisa, lakini bado walicheza na kuruka kusherehekea mafanikio yao.

Viburudisho viliwangoja katika Kanisa Katoliki la St Theresa la Juba, ambapo karamu ya kuwakaribisha pia ilikuwa inafanyika. Hujaji mmoja, ambaye alikuwa akitoa machozi alipokuwa akiwasili, alidokeza matatizo ambayo miaka ya mapigano imeleta nchini humu.

Kanisa hilo linaonekana kuwa ishara ya matumaini kwa wengi nchini Sudan Kusini. Ni mahali ambapo wengi waliokimbia mapigano ya nchi hiyo hutafuta kimbilio.

Papa Francis yuko ktika nchi hiyo kwa ziara ya siku tatu na atafanya Misa kubwa siku ya Jumapili hii.

Chanzo: Bbc