Kundi la pili la wanajeshi wa Kenya wanatarajiwa kuwasili Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo leo. Wao ni sehemu ya kikosi cha kikanda kilichotumwa kwa misheni ya kulinda amani mashariki mwa nchi.
Makundi yenye silaha yameongeza mashambulizi katika miezi ya hivi karibuni na kuibua wasiwasi kuhusu tishio wanalotoa kwa usalama wa eneo hilo.
Zaidi ya wanajeshi 900 wa Kenya watakuwa na makao yao karibu na mji wa Goma katika eneo hilo lenye hali tete.
Wanaungana na wanajeshi wa Burundi ambao wamekuwa wakifanya kazi katika jimbo la Kivu Kusini tangu Agosti.
Watasaidia jeshi la Congo kupambana na waasi ambao wamefanya uharibifu katika mwaka uliopita.
Wakiongozwa na kundi la M23, wameteka maeneo zaidi katika miezi ya hivi karibuni na kuwahamisha maelfu ya watu.
Serikali ya Congo inatazamiwa kuanza tena mazungumzo na wawakilishi wa makundi mbalimbali yenye silaha baadaye mwezi huu katika mji mkuu wa Kenya Nairobi.