Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kundi la M23 lazidi kuisumbua DR Congo

M23 Pic Data Kundi la M23 lazidi kuisumbua DR Congo

Fri, 24 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati ikifikiriwa kuwa hali imeanza kuwa shwari mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Novemba 8, 2021 kulizuka mapigano makali yaliyosababisha raia kadhaa wa nchi hiyo kupoteza maisha na wengine kukimbilia Uganda.

Huku Serikali ya Uganda ikithibitisha mapigano hayo kutokea kwenye maeneo ya mji wa Bunagana kwenye mpaka wa Kusini Magharibi, mashirika mawili, lile la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) na la Msalaba Mwekundu yalihofia kuwa yasingeweza kuwahudumia wakimbizi hao, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Wakimbizi hao walieleza kuwa wamekimbia mapigano yaliyozuka nchini kwao ambayo yalikuwa ni kati ya majeshi ya Serikali ya DRC na kundi la wapiganaji wa M23.

Eneo kulikozuka mapigano hayo ni jirani kabisa na makutano ya mipaka ya Uganda, Rwanda na DRC, ikimaanisha kuwa baadhi ya wakimbizi wangeweza kukimbilia Rwanda. Hofu kwa upande wa Uganda ilikuwa ni uwekezano wa wapiganaji kuingia ndani ya mipaka yake na hivyo majeshi yake yaliweka doria na kuwachuja wakimbizi waliokuwa wanaingia nchini humo.

Tofauti na ilivyokuwa awali kwa Uganda na Rwanda kushutumiwa kulisaidia kundi la M23, safari hii Rwanda ilidai wapiganaji wa kundi hilo waliokabiliana na majeshi ya DRC walitokea Uganda, jambo ambalo Uganda ilikanusha vikali.

Msemaji wa jeshi nchini Uganda alithibitisha kwamba kuna kundi la wapiganaji wa M23 nchini humo kama wakimbizi na akasisitiza kuwa waliondolewa kutoka eneo la mzozo kwenye mpaka na DRC wakapelekwa kambi za wakimbizi Kaskazini mwa Uganda mwaka 2017.

Advertisement Taarifa rasmi iliyotolewa na Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF), wapiganaji waliokabiliana na majeshi ya DRC hawakutokea Rwanda kama ilivyodaiwa, bali walitokea Uganda ambako wengine walikuwa wamehifadhiwa tangu mwaka 2013.

Kufikia mwaka huu, ikiwa ni miaka kumi tangu kuanzishwa kwa kundi la M23, hali nchini DRC haijabadilika kuhusu usalama unaohatarishwa na kundi hilo ambalo awali lilifikiriwa kuwa limetokomezwa.

Asubuhi ya Jumatatu ya Machi 28 mwaka huu, kulishuhudiwa mapambano mengine makali katika vijiji kadhaa vya mkoa wa Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini baina ya jeshi la DRC na waasi wa M23.

Maelfu ya wakimbizi kutoka katika baadhi ya vijiji vya kando na milima ya Chanzu na Runyoni walionekana tangu asubuhi ya siku hiyo wakivuka mpaka kuelekea nchi jirani ya uganda kutokana na mapigano makali kati ya jeshi la DRC na kundi la waasi wa M23.

Waasi hao waliteka upya milima ya Runyoni na Chanzu wilayani Rutshuru, ambayo walikuwa wanatumia kama ngome yao kuu chini ya Kamanda Sultani Makenga mwaka wa 2012.

Kuzuka upya mapigano haya kati ya pande zote hizo mbili kuliwatia hofu wanaharakati wa haki za binadamu ambao waliitaka jumuiya ya kimataifa kuingilia kati mzozo huo unaoweza kuyaathiri mataifa jirani.

Mara kwa mara waasi hao wamekuwa wakiishutumu Serikali kwa kuvunja makubaliano kati yao ambayo yalikuwa njia pekee ya kuleta amani. Kurejea kwa kundi la M23 kuliripotiwa wakati Serikali ya Rais Felix Tshisekedi wa DRC ikipambana na waasi wa Allied Democratic Forces (ADF) kutoka Uganda katika wilaya ya Beni na Ituri, operesheni ambazo hadi sasa hazijaleta mafanikio ya kujivunia.

ADF ni kundi la waasi wa Kiislamu, lenye chimbuko lake nchini Uganda lakini kwa sasa limejichimbia mashariki mwa DRC. Kundi hili la uasi lilianzishwa miaka ya 1990 kwa lengo la kuung’oa utawala wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda lakini lilikimbizwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF) na kukimbilia DRC.

Jumapili Aprili 10 mwaka huu, waasi wa M23 walitangaza kuondoka kutoka vijiji walivyoviteka mashariki mwa DRC wiki iliyotangulia baada ya makabiliano na vikosi vya Serikali katika wilaya ya Rutshuru. Mapigano kati ya waasi hao na wanajeshi wa DRC yalipamba moto siku nne zilizokuwa zimepita baada ya siku kadhaa za utulivu na waasi wa M23 kuchukua udhibiti wa vijiji kadhaa vya mkoa wa Kivu Kaskazini.

Kundi hilo lilisema limefikia uamuzi huo wa kujiondoa mara moja kwenye maeneo mapya waliyoteka ili kutoa fursa ya kushughulikia masuala yake kupitia majadiliano na Serikali ya DRC.

Taarifa ya kundi hilo ilisema M23 haikuwa na nia ya kuteka maeneo ili kuyaendesha, bali dhamira yao ni kufikia suluhisho la amani la mzozo huo. Lakini wengi, wakiwamo maofisa wa DRC, hawakuamini iwapo M23 imeondoka kweli au ni hadaa.

Waasi walikuwa wamevikalia vijiji vya Gisiza, Gasiza, Bugusa, Bikende-Bugusa, Kinyamahura, Rwambeho, Tshengerero, Rubavu na Basare na waliendelea kuteka vijiji vya Runyoni na Tchanzu. Na huo haukuwa mwisho wa kuteka vijiji vingine. M23 liliendelea na utekaji huo huku likiishutumu Serikali kwa kukiuka makubaliano mwaka uliopita na hivyo kurejea kupigana. Hii ni kabla na baada ya kuanzisha upya mashambulizi yao mwishoni mwa Machi mwaka huu.

Wakati M23 wakisema wanajiondoa katika vijiji walivyoteka kuruhusu majadiliano na Serikali ya Tshisekedi, Aprili 11 mwaka huu, waasi wa ADF nchini DRC walidaiwa kufanya mauaji ya zaidi ya watu 30 katika vijiji vya Machwalo, Shaurimoya na Mangusu wilayani Irumu katika mkoa wa Ituri.

Mauaji hayo yalitokea wakati majeshi ya DRC na yale ya Uganda yakikabiliana na waasi hao katika eneo la Beni na Irumu.

Mara baada ya mauaji hayo, msemaji wa jeshi la DRC katika mkoa wa Ituri, Luteni Jules Ngongo, alitangaza kuendelea kwa operesheni za kijeshi kwa nia ya kuyaondoa makundi ya waasi katika maeneo hayo. Aliwataka wakazi wa eneo hilo kubakia majumbani mwao kwa utulivu wakati jeshi likiendeleza mapambano yake ya kuvitokomeza vikundi hivyo vinavyotekeleza mauaji ya raia na uporaji mali.

Wakati hayo yakiendelea, Jumatatu ya Mei 23 ilitolewa ripoti mpya ikionyesha kuwa zaidi ya watu 15,000 wamepoteza maisha katika mauaji ya kila mara yaliyofanyika mashariki ya DRC tangu kuanza kwa mzozo huo upya, hususan katika mikoa ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.

Lakini usiku wa kuamkia siku ya kutolewa kwa ripoti hiyo, Jumapili ya Mei 10, mapambano yaliripotiwa kati ya jeshi la Serikali ya DRC (FARDC) na waasi wa M23 katika eneo la Ruthshuru, eneo ambalo si mbali na nchi ya Rwanda.

Katika mkoa wa Kivu kusini pia mapambano makali yaliripotiwa siku hiyo hiyo huko Bigaragara katika maeneo ya Minembwe.

Wakati mapigano yakizuka wilaya za Rutshuru na Nyiragongo kati ya kundi la M23 na wanajeshi wa serikali ya DRC, uhusiano kati ya Rwanda na DRC unazidi kuzorota. Kujua kilichojiri tukutane toleo lijalo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live