Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kufunguliwa mipaka Burundi kukuze biashara

Eafce6295a1ebf4813aeaa491f230468.png Kufunguliwa mipaka Burundi kukuze biashara

Tue, 22 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

BURUNDI imetangaza kufungua mipaka yake na Tanzania ambayo ilikuwa imefungwa.

Mipaka iliyofunguliwa ni ya Kobero-Kabanga na Mugina ambayo ilikuwa imefungwa kutokana hatua zilizochukuliwa na serikali ya Burundi kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa hatari wa covidi-19.

Kufunguliwa kwa mipaka hiyo ni hatua nzuri ambayo itasaidia kuongeza biashara kati ya nchi hizo mbili ambazo zilikuwa zimefifia kwa muda kutokana na kutokuwapo kwa muingiliano wa wananchi wa nchi hizo mbili jirani.

Tanzania na Burundi kwa muda mrefu zimekuwa na muingiliano mkubwa wa wananchi wake hasa katika masuala ya kibiashara na kijamii, hususani kwenye mikoa inayopakana, hivyo kufungwa kwa mipaka hiyo kulikuwa na athari kubwa.

Kutokana na mipaka hiyo kufunguliwa, tunatoa rai kwa Watanzania kutumia fursa hiyo kufanya biashara na wenzao wa Burundi ili kujiongezea kipato.

Kwa mujibu wa Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Dk Jilly Maleko, nchi hiyo imefungua mipaka yake kwa ajili ya kurahisisha muingiliano wa watu na bidhaa.

Amezitaja bidhaa zinazohitajika kwa wingi Burundi ni pamoja na mchele, mtama mweupe, mahindi na unga wa mahindi, mihogo iliyokaushwa (udaga) na unga wa mhogo na kuwataka Watanzania kuchangamkia fursa hizo.

Bidhaa nyingine ni maharage, mafuta ya kupikia, chumvi yenye madini joto, mvinyo, vifaa vya ujenzi (saruji, vigae, mabati, nondo na nyinginezo.

Ukiangalia takwimu utaona thamani ya bidhaa za Burundi zilizouzwa Tanzania mwaka 2019 ni Sh milioni 831.4 na Tanzania iliuza nchini humo bidhaa zenye thamani ya Sh bilioni 200.18.

Aidha, kuanzia mwaka 2015 hadi 2019, Tanzania na Burundi zilifanya biashara ya Sh bilioni 619.9, ambayo ni wastani wa Sh bilioni 123.9 kwa mwaka. Hii ni ishara kuwa soko la bidhaa za Tanzania nchini Rwanda ni kubwa.

Watanzania wana fursa kubwa ya kuuza bidhaa mbalimbali nchini humo ambazo kwa hapa nchini zinapatikana kwa wingi.

Kama tulivyosema awali, mahitaji wa bidhaa hizo ni makubwa mno katika nchi hiyo ya jirani, hivyo Watanzania wasilaze damu bali wachangamkie fursa hiyo kwa kufanya biashara kwa wingi.

Tunatoa wito kwa Watanzania hasa wafanyabiashara wakubwa kwa wadogo kusafirisha na kuuza kwa wingi bidhaa mbalimbali nchini humo ili kujipatia kipato kizuri kwa faida yao binafsi na kuliingizia taifa mapato kupitia tozo mbalimbali.

Ni imani yetu kuwa, kufunguliwa kwa mipaka ya Burundi kitakuwa kichocheo kikubwa cha kukuza baishara kati ya mataifa hayo mawili jirani na marafiki wa muda mrefu.

Chanzo: www.habarileo.co.tz