Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kisa cha mke wa Raila kuzomewa

Mke Wa Railapic Data Kisa cha mke wa Raila kuzomewa

Tue, 29 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ida Odinga, mke wa Kiongozi wa Upinzani Kenya, Raila Odinga amekutana na fadhaa ya haja, baada ya kuzomewa alipokuwa anatoa hotuba kwenye kongamano la Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Kenya (CWA), Dayosisi ya Meru.

Mkutano wa Umoja wa Wanawake Wakatoliki ulifanyika jana, Meru na kuhudhuriwa na wanawake wengi wa jumuiya hiyo, wakiwemo wanasiasa wenye misimamo inayopingana na Raila.

Wanasiasa wengine waliohudhuriwa kongamano hilo ni mbunge wa Imenti Kaskazini, Rahim Dawood (Chama cha Jubilee), mbunge wa kuteuliwa, Halima Mucheke na Seneta Mithika Linturi, ambaye katika uchaguzi ujao anagombea ugavana wa Meru kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Sababu ya Ida kuzomewa bila shaka ni kitendo cha siasa kutawala kwenye mikusanyiko wa kidini, kwani watu wasiofungamana na mrengo wa Raila, waliona kama mwanamke alipewa nafasi ya kuhutubia ili kumsafishia mume wake njia ya kisiasa.

Mkutano ulifanyika katika Shule ya Msingi Consolata, Meru na kuhudhuriwa na wanawake kwa mamia. Hali ilikuwa mbaya baada ya mratibu wa CWA, Dayosisi ya Meru, Gemma Kathure, kutangaza kuwa Ida ndiye mtu pekee aliyepaswa kutoa hotuba katika mkusanyiko huo.

Kauli hiyo ya Kathure iliwafadhaisha baadhi ya wahudhuriaji, hususan wasiokubaliana na Raila, hivyo kuanza zomeazomea na pale Ida alipokuwa akitoa hotuba yake, sauti za kumzomea ziliongezeka na kusababisha ashindwe kuhutubia kwa utulivu.

Advertisement Ilimlazimu Kathure kila mara asimame katikati ya hotuba ya Ida ili kuwatuliza watu ili kumruhusu aendelee kuhutubia. Pamoja na jitihada nyingi za Kathure, bado hali iliendelea kuwa mbaya. Mkutano huo ulifika mwisho katika hali iliyotawaliwa na sintofahamu.

Raila ni Kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM). Kuelekea uchaguzi mkuu ujao nchini Kenya, ameunda ushirika wa kisiasa unaoitwa Azimio la Umoja na yeye ndiye kiongozi wa mungano huo, unaungwa mkono na chama tawala cha Jubilee.

Katika uchaguzi mkuu ujao, unaotarajiwa kufanyika Agosti 9, mwaka huu, Raila anachuana na vikali na Naibu Rais, William Ruto aliyejitoa katika chama cha Jubilee na kuunda chama kipya cha UDA, huku akiongoza ushirika wa kisiasa unaoitwa Kenya Kwanza.

Rahim Dawood, yeye ameshajipambanua waziwazi kuwa upande wa Ruto, wakati Seneta Linturi, kwa kuwa anagombea ugavana wa Meru kupitia UDA, maana yake pia yupo upande wa Kenya Kwanza.

“Nipo hapa kama mwanamke na hamtakiwi kukataa kunisikiliza kwa sababu mimi ni mke wa Raila Odinga. Unapojumuika kwenye mkutano wa Umoja wa Wanawake wa Kanisa Katoliki, maana yake wewe ni Mkristo,” alisema Ida baada ya kuona anazidi kuzomewa.

Ida aliongeza: “Imani ya Ukristo haipaswi kuwa kwenye mwonekano wa nje, bali inatakiwa ianzie moyoni. Nawaomba wanawake wenzangu wa Kenya, tuendelee kuiombea Kenya yetu, tuombe umoja na mshikamano wa kitaifa, kuliko kugawanywa kwa sababu za kisiasa.”

Kuna wakati, ili kutuliza hali ya hewa, ilibidi Kathure amtoe nje mwanasiasa mmoja mwanamke mwenyeji wa Meru, na kumtuhumu kuwa ndiye alikuwa anaanzisha uchochezi kwa kuhamasisha wanawake kumzomea Ida.

Hali ilipokuwa mbaya zaidi, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Joseph (kanisa Kuu), David Kaberia aliingilia kati na kuwaambia wanasiasa akiwemo Seneta Linturi, kutii mwongozo wa kanisa, unaotaka waumini kupendana na kutendeana kama wanafamilia.

Hata hivyo, lawama kubwa ilibaki kwa Kathure kwamba alifanya ubaguzi kanisani kwa kumpa mtu mmoja tu nafasi ya kuongea na kuwanyima wengine, kitu ambacho ni kinyume na mwongozo wa kanisa, unaoelekeza Wakristo kutendeana kwa usawa na upendo.

Kathure katika utetezi wake, alisema kongamano la Umoja wa Wanawake wa Kanisa Katoliki, Meru, shabaha yake haikuwa ya kisiasa, isipokuwa lengo lilikuwa kufanya sala na kuwaomba wanawake kujiamini na kumpigia kura ambaye wangeona anafaa.

Upande wa Seneta Linturi, alishauri kuwe na uvumilivu wa kisiasa na kubainisha kuwa wanasiasa wote wanatakiwa kupewa nafasi ya kuzungumza kwa usawa na watu wasinyime fursa ya kuwasikiliza wanasiasa wanaowapenda na kuwaunga mkono.

“Sisi kama jamii ya Meru, tunatakiwa kuwakaribisha watu wote. Tunapaswa kuwapa nafasi ya kuzungumza,” alisema Seneta Linturi na kauli yake kuungwa mkono na watu waliochukizwa na kitendo cha Kathure kumpa nafasi ya upendeleo Ida na kuwanyima wanasiasa wengine waliokuwa kanisani.

Spika wa Bunge la Kaunti ya Meru, Joseph Kaberia, aliwalaumu wote waliomzomea Ida, akasema: “Watu wanapaswa kuwasikiliza wanasiasa wote. Njia bora ya kupinga ni kumpigia kura mtu unayemuunga mkono. Pia, wanasiasa wanapaswa kuheshimu watu pale hotuba zao zinapokataliwa.”

Tamthiliya ilizidi kunoga pale mtia nia ya ubunge jimbo la Imenti Kaskazini, Beatrice Karwitha alipoanzisha zogo dhidi ya mbunge wa sasa wa jimbo hilo, Dawood.

Beatrice alimlaumu Dawood kuwa alishirikiana na mbunge wa Kaunti ya Meru, Elias Murega kumnyima na yeye nafasi ya kuzungumza. Baadaye Beatrice alitolewa nje na walinzi.

Upande mwingine, Dawood alilalamika kuwa alipigwa ngumi ya mgongoni, akaongeza kwamba Tume ya Taifa ya Mshikamano na Ushirikiano (NCIC), inatakiwa kulifanyia kazi tukio hilo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live