Kapteni wa jeshi aliyeongoza mapinduzi ya hivi punde zaidi nchini Burkina Faso ameteuliwa kuwa rais wa muda hadi uchaguzi utakapofanyika Julai 2024. Jukwaa la kitaifa lilitangaza kwamba Kapteni Ibrahim Traoré hataruhusiwa kuingilia katika uchaguzi.
Alinyakua mamlaka wiki mbili zilizopita kutoka kwa Luteni Jenerali Paul-Henri Damiba, ambaye alifanya mapinduzi mwezi Januari akishutumu mamlaka kwa kushindwa kukabiliana na wanamgambo wa Kiislamu.
Uasi ulizidi baada ya jenerali huyo kutwaa mamlaka, jambo lililosababisha Kapteni Traoré kumwondoa kwa nguvu.
Traore, mwenye umri wa miaka 34, alianza kazi yake ya kijeshi mwaka wa 2009 na amehudumu katika vikosi mbalimbali mashariki na kaskazini mwa Burkina Faso.