Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kiongozi wa kijeshi Chad ateuliwa kuwania Urais

Gene Debyy (17).jpeg Kiongozi wa kijeshi Chad ateuliwa kuwania Urais

Sun, 14 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais wa mpito wa Chad, Jenerali Mahamat Idriss Deby Itno ameteuliwa na chama chake cha MPS kuwa mgombea wa urais utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Uteuzi uliofanyika Jumamosi Januari 13, 2024 katika mkutano mkuu wa chama unakuja baada ya kura ya maoni ya Desemba kuidhinisha Katiba mpya ambayo watawala wa kijeshi wa nchi hiyo waliipigia debe kama hatua muhimu katika njia ya kurudi kwa utawala wa kiraia.

Katiba hiyo pia iliungwa mkono na kiongozi mkuu wa upinzani, Succes Masra aliyeteuliwa kuwa Waziri Mkuu mapema mwezi huu.

Hata hivyo, vyama vya upinzani na asasi za kiraia vilitoa wito wa kususia kura ya maoni, vikisema ilikuwa ni onyesho tu la kuandaa njia ya kuchaguliwa kwa Deby, kuendeleza utawala wa familia ya Deby wa miaka 33.

Deby (37) alitangazwa kuwa rais wa mpito wa kijeshi Aprili 2021 baada ya kifo cha baba yake Idriss Deby Itno, aliyeuawa na waasi akiwa njiani kuelekea mstari wa mbele kwenye mapigano. Hayati Deby alikuwa ameitawala Chad kwa mkono wa chuma kwa zaidi ya miaka 30.

“Rais wa mpito, Mahamat Idriss Deby Itno, ameteuliwa kuwa Rais wa heshima na mgombea mtarajiwa wa chama cha MPS katika uchaguzi ujao wa urais kwa azimio la wabunge,” amesema Mariam Djimet Ibet, mkuu wa kamati ya Bunge ya chama cha MPS.

Jenerali huyo kijana, awali aliahidi kuandaa uchaguzi baada ya kipindi cha mpito cha miezi 18, lakini utawala wake baadaye uliongeza kipindi cha mpito kwa miaka miwili na kumruhusu kuwania uchaguzi wa urais ambao sasa umepangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka 2024.

Oktoba 20, 2022, kati ya vijana 100 na 300 waliuawa kwa kupigwa risasi na polisi na wanajeshi huko N'Djamena, kwa mujibu wa upinzani na NGO za kitaifa na kimataifa.

Walikuwa wakiandamana kwa amani kupinga kuongezwa miaka miwili kwa Serikali ya mpito.

Wengine zaidi ya 1,000 walifungwa kabla ya kusamehewa baadaye huku makumi wengine wakiteswa au kutoweka, kwa mujibu wa NGO na vyama vya upinzani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live